Majukwaa ya kidijitali yameleta mapinduzi makubwa katika namna biashara zinavyofanyika. Kupitia mitandao ya kijamii kama Instagram, Facebook, na WhatsApp, wafanyabiashara wanaweza kuwafikia wateja wengi kwa haraka na gharama nafuu.
Badala ya kuwa na duka la kawaida linalohitaji kodi na gharama za uendeshaji, sasa mtu anaweza kuuza bidhaa au huduma akiwa nyumbani kupitia simu ya mkononi.
Aidha, majukwaa kama Piku yameboresha upatikanaji wa masoko ya bidhaa kutoka mikoa mbalimbali nchini hali inayoongeza ushindani wa bei na ubora wa huduma kwa wateja.
Majukwaa ya kidijitali yanafikia idadi kubwa ya watu duniani kwani kufikia mwaka 2025, takwimu zinaonyesha kuwa watumiaji wa intaneti duniani wamefikia zaidi ya watu bilioni 5.3, kati ya jumla ya watu takribani bilioni 8.
Hii inaonyesha kuwa majukwaa ya kidijitali yanafikia zaidi ya asilimia 65 ya watu wote duniani, na idadi hii inaendelea kukua kila mwaka
Kwa kutambua hilo, Mwananchi imefanya mahojiano Mahojiano maalumu na Sia Malewas, Meneja Uendeshaji wa Biashara Piku, moja ya jukwaa la biashara la kidijitali ili kujua mengi. Fuatilia mahojiano haya:
Wazo la Piku lilianzia wapi?
Jibu: Wazo lilianza kwenye darasa la ‘combinatorics’ tulikutana na waanzilishi mbalimbali tuliosoma Computer Science. Wazo la Piku ni jukwaa linalotumia masomo mbalimbali ambayo tuliyapenda. Masomo ambayo yanachangamsha akili.
Pia, lilitokana na kipindi kutoka Marekani ambacho waangaliaji wanapewa bidhaa kisha waambiwa wataje bei yake ambapo anayekaribia bei yake ndiye anayeshinda. Ni juu ya kumpa mtu matumaini. Lengo la Piku ni kwenda Afrika nzima.
Piku imekuja kuwaletea bidhaa nzuri kwa dau dogo ya kipekee. Buku tu inakuwezesha wewe kipata bidhaa unayoipenda.
Kitu gani kinafanya Piku ionekane tofauti na majukwaa mengine ya kimtandao?
Jibu: Kwanza, ndani ya Piku tunatarajia mtu anaweza akafungua duka lake, mfano duka la vipodozi. Sasa, yeye mwenyewe anaweza akasema pafyumu zake tano akaziweka kwenye mnada akajitangaza zaidi.
Ila kwa sasa hivi tunaanza na mnada, baada ya miezi kadhaa tutafungua jukwaa letu la mauzo. Kiteknolojia, tumeleta teknolojia nyingi sana hapa Tanzania. Ubunifu wetu ni wa ukweli kwa sababu vitu vyetu viko tofauti.
Piku inamchango gani kwenye uchumi wa Tanzania?
Jibu: Piku itaajiri zaidi ya watu 15 wachambuzi wa data. Upande wa mfumo ya kiteknolojia, itaajiri vijana ambao watasimamia code, kile chombo kitakachoshikilia Piku nacho kitatoa ajira. Tutakuwa kwenye jengo letu ambalo litatuwezesha kufanya vitu vingi zaidi. Kuna watu wa uzalishaji watakuwa hapo.
Baada ya miaka mitatu, tunataka Piku ijulikane Afrika Mashariki na Magharibi. Tutaipa sifa Tanzania kwa kubuni kitu chenye manufaa kwa Waafrika wote, tutatengeneza ajira.
Kitendo cha kuwa na kampuni nje ya Tanzania na kampuni mama ipo ndani icho kitendo pia kitaleta hela, mapato na pesa za kigeni jambo ambalo Tanzania itapata faida ya kile kitu ilichoanzisha.
Pia, kitendo cha kuja na Piku inaleta uthubutu kwa watu wengine kuweza kujaribu na kubuni vitu ambavyo ni vizuri. Unaondoa ile hali ya kusema hiki kitu hakiwezekani.
Kwanini mtu achague kutumia Piku na si jukwaa lingine?
Jibu: Kwanza hakuna jukwaa lingine zaidi ya Piku. Lengo letu sisi ni kuisambaza Afrika nzima. Pia, kitendo cha kutumia Sh1000 ukashinda vitu vikubwa kama gari, tv na bidhaa nyingine ni jambo la kipekee.
Bidhaa tunazoziweka kwenye Piku kwanza zipo za jinsia zote. Mfano safari za kwenda Dubai, Uturuki, China. Tunavyozidi kukua tunaangalia mahitaji ya wananchi ni yapi, ili kuzidi kuwapa tumaini.
Tumeweka nia kwamba asilimia 35 ya mapato yetu tutayapeleka kwenye (CSR), kurejesha kwa jamii. Tunataka kuanzisha Piku Foundation. Tutapeleka mapato yetu Muhimbili kusaidia watu wasio na uwezo.
Kwa upande wa elimu mfano mtu amesoma vizuri na wazazi wake hawana uwezo wa kumsomesha zaidi basi Piku tutamsomesha. Tunataka zile pesa tunazopata zinarudi kwa jamii.
Hali ya uwekezaji ikoje na je, kuna mipango mingine?
Jibu: Piku imeanza karibu miaka 20 iliyopita. Kulikuwa na mipango mikakati tuliyokuwa tunaisubiri kama kuongezeka kwa watumiaji wa intaneti pamoja na mifumo ya malipo yaani jinsi gani tungeweza kupokea malipo. Mfano sasa hivi kuna malipo ya kidijitali kama control number.
Pia, tulikuwa tunaandika ‘software’ kwa maana tulikuwa tunatengeneza injini za kuchakata data. Tumeweka uwekezaji wa karibu miaka 20 na ukiangalia uwekezaji huu sio chini ya Sh800 milioni.
Kwa miezi mitatu inayokuja tutawekeza Sh120 milioni kwa ajili ya zawadi, pamoja na soko. Tutaangalia soko linataka nini tuongeze pesa au tuongeze zawadi hadi Sh1 bilioni. Sisi hatuna kikomo kama kutoa zawadi kila siku.
Umuhimu wa Piku ni mkubwa kwanza hatuangalii soko la Tanzania tu bali hadi nje ili kurudisha pesa nyumbani.
Je, kwa mtazamo wako, hali ya soko mtandao ikoje kwa sasa nchini?
Jibu: Kuna mwamko kwa kuwa wateja wana mwamko wa malipo ya kimtandao. Kuna watu wananunua vitu kwenye mtandao bila ya kwenda dukani. Kwa upande wa vijana, hii ni fursa kubwa. Mfano kwa wakulima kutumia mitandao na mtu kuanzisha jukwaa na mtandao litakalowasaidia wakulima kupata huduma.
Tathmini ya mwenendo wa uchumi wa kidijitali Tanzania upoje?
Jibu: Kasi nzuri ipo kwenye malipo ya kupokea na kutuma pesa. Nafikiri na benki zibadilike ziige mitandao ya simu. Malipo mengi yanapitia kwenye mitandao ya simu. Piku inaandalia fursa ya kujenga uaminifu kwa watu.
Changamoto gani ambazo bado zinakwamisha ukuaji sekta ya uchumi wa kidijitali Tanzania?
Jibu: Vifaa vinavyotumika kwenye mitandao kwa mfano simu ziko nyingi za aina tofauti tofauti nyingine za bei rahisi na bei ghali. Kwenye mnyororo wa upande wa simu upo kwnye kupiga na kupokea na si upande wa data.