Waziri wa Zimbabwe asisitiza mshikamano kufikia malengo ya SADC

Antananarivo. Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Zimbabwe, Profesa Amon Murwira amezisisitiza kuwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili zifikie safari ya ukombozi wa kiuchumi, lazima kuwe na mshikamano wa kutekeleza malengo waliyojiwekea.

Profesa Murwira ameyasema hayo leo Jumanne Agosti 12, 2025, kabla ya kukabidhi uenyekiti wa Baraza la Mawaziri la SADC kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Rasata Rafaravavitafika, jijini Antananarivo.

Katika kikao hicho cha Baraza la Mawaziri, Tanzania inawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.

Ajenda inayojadiliwa kwenye kikao hicho ni maandalizi ya mkutano wa 45 wa wakuu wa nchi wa SADC, uliopangwa kufanyika Agosti 17, 2025.

Profesa Murwira amesema safari yoyote haikosi changamoto na ametumia jukwaa hilo kuwatahadharisha washiriki wa mkutano huo kuwa changamoto zisiwe sababu za kutofikiwa malengo mazuri yaliyoanzisha SADC.

“SADC ilianzishwa kwa lengo la mtangamano wa kikanda, nchi wanachama zinatakiwa zikumbuke hili wakati wote na kukumbuka dhamira njema ya waasisi wa jumuiya kama vile wakiwamo hayati Mwalimu Julius Nyerere, Robert Mugabe na Kenneth Kaunda,” amesema.

Profesa huyo amehitimisha hotuba yake kwa kupongeza jitihada zinazochukuliwa na nchi wanachama za kuimarisha mtangamano kama vile uondoaji wa sharti la viza na usuluhishi wa mgogoro wa mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambao athari zake zinazikumba nchi zote za SADC.

Naye Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi amewakumbusha washiriki wa mkutano huo juu ya dira ya maendeleo ya jumuiya hiyo, ambayo imejikita katika maendeleo ya viwanda, kupanua mtangamano wa kikanda, biashara na masoko.

Amesema lengo la mkutano huo ni kupitia utekelezaji wa dira hiyo kwa mwaka mmoja uliopita, mafanikio yaliyopatikana na kutafuta suluhu kwa pamoja katika changamoto zilizojitokeza.

Amesisitiza kuwa mkutano huo unafanyika wakati dunia inashuhudia changamoto mbalimbali kama vile mabadiliko ya siasa za kimataifa, ongezeko la kodi katika biashara, na kupungua kwa kiasi kikubwa kwa misaada kutoka kwa wahisani.

Hayo yote, amesema, yameathiri mtiririko wa biashara na uwekezaji katika kanda, utaratibu uliozoeleka wa kufanya biashara na ugharamiaji wa miradi, changamoto ambazo zinaonekana kurejesha nyuma jitihada za SADC.

“Moja ya malengo ya mkakati wa viwanda wa SADC 2015–2063 umetoa msisitizo mkubwa wa uendelezaji wa biashara ndogo na za kati (SMEs), hasa kutokana na idadi kubwa ya vijana na wanawake kujihusisha na sekta hiyo,” amesema.