UNAJUA nini kinaendelea Jangwani? Kwa mashabiki wa kikosi cha Yanga wanaambiwa kwamba watarajia vitu vingi vitakavyowapa vaibu la kutosha msimu ujao, huku kukiwa na vyuma vya maana tu ambavyo vimeshaanza kujifua ili kutetea ubingwa wa mashindano mbalimbali.
Ni katikati ya vaibu la tizi linaloendelea hapo ndipo ilipo siri nyingine ambayo ya mafanikio ya chama hilo ambalo katika misimu minne mfululizo limewaburuza wapinzani wake katika mashindano makubwa hapa nchini kuambua patupu, jambo ambalo linawaumiza vichwa.
Sasa sikia hii! Beki wa zamani wa Yanga, Joyce Lomalisa anayekipiga kwa sasa Wiliete Benguela ya Angola ameitabiria makubwa na kuwapa nafasi kubwa vijana hao wa Jangwani kuvuka raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sababu ya uzoefu mkubwa walionao na hata wa wachezaji.
Yanga imepangwa kukutana na Benguela katika mechi za raundi ya kwanza baada ya droo ya michuano ya klabu kwa msimu wa 2025-2026, ikianzia ugenini na kumalizia nyumbani na hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Lomalisa kukutana na mabosi wake hao wa zamani katika michuano ya CAF.
Lomalisa aliyeitumikia Yanga kwa misimu miwili akitwaa mataji mawili na kuvaa medali ya CAF baada ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ameiambia Mwanaspoti kuwa Wiliete Benguela ni timu nzuri, lakini haina uzoefu na wachezaji wenye uwezo kuwazidi waliopo Yanga.
“Naipa nafasi kubwa Yanga kutinga hatua inayofuata kutokana na kuwa na wachezaji wengi bora ambao pia wanauzoefu mkubwa tofauti ta Wiliete ambayo ndio mara yao ya kwanza kushiriki mashindano hayo na ina wachezaji wengi ambao ni vijana hawana uzoefu,” amesema na kuongeza:
“Yanga ukiiangalia mchezaji mmoja mmoja ni bora zaidi na kuna wachezaji ambao wana zaidi ya misimu mitatu wameshiriki mashindano makubwa na kuivusha nafasi tofauti timu hiyo hivyo ni wazi kuwa wana uzoefu mkubwa wataipambania iweze kufanya vizuri na kutinga hatua inayofuata.”
Lomalisa amesema hayupo timu hiyo kwa sasa, lakini anaifahamu kwa sababu ameitumikia kwa msimu mmoja kabla ya kuondoka na kujiunga na Kabuscorp SC ya Angola ambayo pia amemaliza nayo mkataba akisema ni nafasi ya wachezaji wa Yanga kufanya jambo kubwa kulingana na uzoefu walionao. Awali aliichezea pia G.D. Sagrada Esperanca.
“Nina imani kubwa na nyota waliopo Yanga wengi wana vipaji vikubwa naamini sasa ni muda wao wasisi kufanya vizuri kwenye mchezo huo na hatimaye kutinga hatua inayofuata.”
Lomalisa alijiunga na Yanga chini ya Nasreddine Nabi msimu wa 2021/22 amepita pia chini ya Miguel Gamondi msimu mmoja 2023/24. Yanga inatarajia kuanzia ugenini mchezo wa awali dhidi ya Wiliete Benguela utachezwa kati ya Septemba 19 hadi 21 huku mchezo wa nyumbani ukitarajiwa kupigwa Septemba 26-28.