Waarabu wa Mzize, waibomoa RS Berkane

ILE klabu inayomtaka mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize haitanii inakusanya mastaa hasa na sasa imepepelea kilio RS Berkane, ikiondoka na nahodha wa timu hiyo.

Umm Salal ya Qatar imemng’oa nahodha huyo wa Berkane, Issoufou Dayo aliyekuwa staa mkubwa wa mabingwa hao wa Morocco.

Dayo (34) anayecheza beki wa kati, ndiye aliyeiongoza Berkane kuchukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita kwa kuifunga Simba kwa jumla ya mabao 3-1.

Beki hiyo raia wa Burkina Faso, amesaini mkataba wa miaka miwili kuwatumikia Waarabu hao wa Qatar, timu hiyo ikiunda kikosi kipya, ambapo mbali na beki huyo imemsajili piavkiungo mkabaji,  Jean Eudes raia wa Ivory Coast.

Salal ilimpa Mzize ofa kubwa ambapo klabu ya Yanga ilikuwa ivune kiasi cha Dola 900,000 (Tsh 2.2 Bilioni) kwa awamu mbili.

Hata hivyo, ofa hiyo iliyozusha mvutano mkubwa kati ya Yanga na wasimamizi wa mshambuliaji huyo aliyemaliza msimu uliopita na mabao 14 ya Ligi Kuu, inaelezwa kuna uwezekano wa kukataliwa na kuchukuliwa ofa nyingine ya Esperance de Tunis ya Tunisia.