Dar es Salaam. Washtakiwa saba wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka 20 yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7 bilioni kwa udanganyifu mali ya benki ya Equity Tanzania Limited.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao na kisha kuunganishwa na wenzao wanne ambao ni Jasmine Elphas ambaye alikuwa ni ofisa wa benki ya Equity makao makuu na mfanyabiashara Fredrick Elphas Ogenga.
Yupo pia, Caroline Masayanyika na Lilian Koka, wote walikuwa maofisa wa benki hiyo kutoka makao makuu ambao walisomewa mashtaka yao Julai 28, 2025.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Eric Shija akishirikiana na Eric Davies, ametaja majina washtakiwa wapya walisomewa mashtaka yao leo Jumanne Agosti 12, 2025 kuwa ni
Halifa Maina, Kaizilege Mohamed, Daudi Fata, Mrisho Mrisho, Neema Paul, Claude Beda na Jefferson Ogenga, wote ni wafanyabiashara.
Awali, kesi hiyo ilikuwa na mashtaka manne likiwemo la kuongoza genge na wizi wa Sh4.4 bilioni mali ya benki hiyo, lakini leo washtakiwa hao wameongezewa mashtaka na kufikia 20.
Wakili Shija amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 18447 ya mwaka 2025.
Kabla ya kuwasomewa mashtaka hayo, Hakimu Nyaki alisema, washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote mahakamani hapo kwa sababu Mahakama ya Kisutu, haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.
Akiwasomea mashtaka yao, wakili Shija alidai kati ya Agosti 30, 2024 hadi Juni 28, 2025 katika maeneo tofauti ndani ya jijini Dar es Salaam, waliongoza genge la uhalifu na kujipatia Sh5.7 bilioni mali ya benki ya Equity Tanzania Limited.
Wakili huyo aliendelea kudai, katika tarehe hizo mshitakiwa Jasmine na Ogenga, wakiwa ndani ya makao makuu ya benki ya Equity iliyopo Ilala, waliiba Sh3.6 bilioni zilizokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), katika akaunti ya clearing and settlement mali ya benki ya Equity.
Aliendelea kudai kuwa mshtakiwa Caroline katika tarehe hizo, akiwa katika makao makuu ya benki ya Equity iliyopo Ilala, aliiba Sh728 milioni mali ya benki hiyo.
Pia ilidaiwa, kati ya Februari 28 na Aprili 2, 2025 makao makuu ya benki hiyo, Lilian aliiba Sh26 milioni kutoka akaunti ya benki hiyo.
Wakili Shija aliendelea kudai, kati ya Januari Mosi hadi Aprili 24, 2025 katika benki hiyo, Maina aliiba Sh101 milioni mali ya benki hiyo.
Ilidaiwa, kati ya Januari 22 hadi Aprili 24, 2025 katika ofisi hizo za benki hiyo Mohamed, aliiba Sh57 milioni, huku Fata akidaiwa kuiba Sh758 milioni, tukio analodaiwa kulitenda kati ya Novemba 2 ,2024 hadi Mei 25, 2025
“Mheshimiwa hakimu, kati ya Januari 9, hadi Mei 25, 2025, makao makuu ya benki ya Equity iliyopo Ilala, Mrisho aliiba Sh211 milioni, mali ya benki hiyo” alidai Shija.
Mahakama hiyo iliendelea kuelezwa kuwa kati ya Januari 9 hadi Mei 28,2025 makao makuu ya benki hiyo, mshtakiwa Neema aliiba Sh32 milioni mali ya benki hiyo.
Vilevile siku na eneo hilohilo, Beda anadaiwa kuiba Sh108 milioni, mali ya benki hiyo.
Pia ilidaiwa, washitakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 10 ya utakatishaji wa fedha walizodaiwa kuiba.
Baada ya kusomwa mashtaka hayo, upande wa mashtaka ulidai upelelezi haujakamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, mawakili wanaowatetea washtakiwa hao Steven Mosha na Meshack Davis waliomba upande wa mashtaka uharakishe upelelezi.
Hakimu Nyaki aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 26, 2026 kwa ajili ya kutajwa.