Hai. Askari wanafunzi 15 wa Shule ya Polisi Tanzania (TPS) Moshi zamani CCP, mkoani Kilimanjaro wamenusurika kifo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na gari aina ya fuso.
Ajali hiyo imetokea leo Agosti 12, 2025 katika eneo la Kwasadala, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro baada ya gari lililobeba askari wanafunzi hao likitokea kambi ya Polisi iliyopo wilayani Siha kugongana uso kwa uso na fuso iliyokuwa ikitokea Wilaya ya Moshi.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo leo Agosti 12,2025 na kueleza kuwa majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Hai kwa matibabu.
“Leo saa tano asubuhi, nimepata taarifa kuwa kuna ajali imetokea eneo la karibu na Kwa Sadala, Wilaya ya Hai iliyosababishwa na magari mawili, Land Cruiser ya Jeshi la Polisi na fuso na kusababisha majeruhi,” amesema RC Babu.
Ameongeza kuwa; “Magari haya yamegongana uso kwa uso ambapo moja lilikiwa linatoka upande wa Moshi na jingine upande wa Bomang’ombe, kwenye gari ya polisi kulikuwa na vijana wetu ambao walikuwa wanatoka kwenye kambi ya Jeshi la Polisi kuja mjini Moshi na fuso lilikuwa kwenye shughuli zake za kawaida.”
Aidha, RC Babu ametoa wito kwa madereva kuwa makini wawapo barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu.
“Niendelee kutoa wito kwa madereva kuwa makini wanapokuwa barabarani, kwani mkoa wetu haujatulia na hizi ajali zinatokea mara kwa mara,” amesema RC Babu.
Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Hai, Dk Emmanuel Minja amesema wamepokea majeruhi 15 na mmoja kati yao amepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya KCMC kwa matibabu zaidi.
“Leo asubuhi tumepokea majeruhi wa ajali 15, katika majeruhi hawa majeruhi mmoja tumempa Rufaa ya kwenda KCMC kwa ajili ya matibabu zaidi, lakini majeruhi 14 wapo hapa wanaendelea kupatiwa matibabu,” amesema Dk Minja.
Aidha, amesema baadhi ya majeruhi wametenguka viungo, kuvunjika mbavu na wengine majeraha kwenye kichwa na sehemu mbalimbali za miili yao.

Dk Minja amesema mpaka sasa wanaendelea vizuri na matibabu baada ya baadhi yao kushonwa na kupatiwa matibabu ya haraka.
“Tunashukuru Mungu hakuna kifo kilichotokea mpaka sasa, na majeruhi wote wanaendelea vizuri na matibabu isipokuwa yule mmoja ambaye amevunjika mbavu tatu na kuwahishwa hospitali ya KCMC,” amesema Dk Minja.
Dereva asimulia ajali ilivyotokea
Akielezea ajali ilivyotokea, dereva wa fuso, Samuel Nkini amesema ajali hiyo imetokea baada ya gari ya polisi kuhama upande wake na kusababisha kugongana uso kwa uso.
“Nimetokea Dar es Salaam na nilikuwa napeleka mzigo Bomang’ombe Wilaya ya Hai, sasa nilipofika hapa gari ya polisi likitokea upande wa Bomang’ombe liliingia upande wangu na kunigonga uso kwa uso kama mnavyoona” amesema Nkini akiwa eneo la tukio.