Familia ya dereva bodaboda aliyetoweka Moshi yamuangukia Rais Samia

Moshi. Wakati Jeshi la Polisi likieleza kuwa linaendelea na uchunguzi kuhusu kutoweka kwa dereva bodaboda Deogratius Shirima (35), mkazi wa Korongoni, Manispaa ya Moshi, familia ya kijana huyo imemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati tukio hilo ili kusaidia kupatikana kwake.

Deogratius alidaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha mnamo Julai 21, 2025, akiwa kazini, na tangu wakati huo hajulikani alipo, hali iliyozua hofu na sintofahamu kwa ndugu na jamaa zake.

Akizungumza na vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (RPC), Simon Maigwa, alithibitisha kupokea taarifa za kutoweka kwa kijana huyo na kueleza kuwa uchunguzi bado unaendelea ili kubaini ukweli wa tukio hilo.

“Taarifa za awali kuhusu kupotea kwa kijana huyo tunazo, na hatua za uchunguzi zinaendelea kufanyika ili kujua kilichotokea,” alisema RPC Maigwa kupitia taarifa iliyotolewa Julai 28, 2025.

Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 12, 2025 mke wa dereva bodaboda huyo, Mariam Abdi amemwomba Rais Samia kuingilia kati tukio hilo ili kuweza kubaini ukweli wake kwani wanaohusishwa na tukio hilo ni askari ambao ni waajiriwa wa Serikali.

“Kama kuna askari wamekamatwa waseme huyu mtu yuko wapi kama wamemuua basi  watupe mtu wetu, tutamzika,” amedai mke wa dereva huyo.

Mke wa dereva bodaboda aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha Moshi, akizungumzia tukio la kutoweka kwa mume wake.

Amesema; “Tunamwomba Rais Samia hili suala aliingilie kati kwa sababu, watu wamekamatwa na wametajana, waseme huyo Deo yuko wapi, wamemuweka wapi? hata kama amekufa watupe tuu tutamzika.”

Mariam amesema kutoonekana kwake kwa siku 22 inawaweka familia katika wakati mgumu na wanashindwa hata kupata usingizi.

“Kinachotuumiza sana familia, ni kwamba pikipiki aliyokuwa akiitumia mume wangu imekutwa nyumbani kwa askari, sasa kinachofanya wanatuzungusha ni nini na ukweli wanaujua na watu wamekamatwa,” amedai.

Mama mzazi wa kijana huyo, Agustina Shirima amesema tukio la kutoweka kwa kijana wake linamnyima usingizi na kushindwa kufanya shughuli zake za kujipatia riziki.

“Tunaomba tuambiwe ukweli kwamba huyu kijana wangu yuko wapi kama ameuawa basi ijulikane, maana tumechoka, Serikali itusaidie jamani, tunashindwa kulala usiku, maana hatujui huyu kijana wetu yupo katika mazingira gani,” amesema.