Dk Biteko: Kuna maisha baada ya uchaguzi

Kagera. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewataka Watanzania kuwapima wagombea wa nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Pia, amesisitiza wawachague viongozi kwa haki ifikapo Oktoba 29, 2025 na katu wasikubali uchaguzi huo mkuu uwagawe.

Dk  Biteko ameyasema hayo leo Jumanne Agosti 12, 2025 alipomuwakilisha Rais, Samia Suluhu Hassan katika kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya kuzaliwa kwa Dayosisi ya Kagera yaliyofanyika katika viwanja vya Kanisa Kuu la Yohana Mbatizaji – Murgwanza, Ngara.

Amesema Watanzania wanayo haki ya kuwapima wagombea kwa matendo yao na hatimaye kutenda haki kwa kufanya uchaguzi wao kwa njia ya demokrasia, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia kampeni za kistaarabu na kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa maadili.

Akiwasilisha salamu za Rais Samia, Biteko amesema anatambua na kuheshimu mchango wa taasisi za dini katika maendeleo ya Taifa.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni mdau wa kujenga, na kila mnachokifanya kinalenga katika maendeleo ya watu, hivyo anaunga mkono jitihada za maendeleo ya wananchi,” amesema Dk Biteko.

Katika kufanikisha azma yake hiyo, Biteko amesema Rais Samia amechangia Sh50 milioni katika harambee ya ujenzi wa kanisa jipya la Anglikana Dayosisi ya Kagera.

Amesisitiza umuhimu wa kila mtu awe sababu ya furaha kwa mwenzake kusudi kila mmoja aishi maisha ya furaha.

Awali, Askofu wa Dayosisi ya Kagera, Darlington Bendankeha aliishukuru Serikali kwa ushirikiano mkubwa inaowapatia katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Askofu Bendankeha amesisitiza kuwa Serikali katika ngazi zote, inatoa ushirikiano na hivyo kufanikisha utekelezaji wa miradi ya afya, elimu kwa maendeleo ya jamii.

Ameiomba Serikali kufanikisha ujenzi wa barabara inayounganisha taasisi mbalimbali za utoaji wa huduma yenye urefu wa mita 900, gari la wagonjwa na mchango wa ujenzi wa kanisa ambalo ujenzi wake unaendelea kwa gharama ya Sh1.18 bilioni.

Kufuatia maombi hayo, Dk Biteko amemwelekeza Mkuu wa Mkoa, Mkuu Wilaya na Wakala wa Barabara mijini na vijijini (Tarura) mkoani Kagera kufanikisha ujenzi wa kipande hicho huku akitoa ahadi ya gari la wagonjwa katika Hospitali ya Murgwanza baada ya kuwasiliana na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama.

Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao, Askofu Bendankeha amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu na kuwachagua viongozi watakao kuja kuchochea maendeleo.

“Tujiandae kushiriki uchaguzi Mkuu ujao, kura yetu ndiyo nguvu ya mabadiliko,” amesema askofu huyo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwassa amelipongeza Kanisa la Anglikana Tanzania kwa huduma mbalimbali za maendeleo inazozitoa kwa jamii mkoani humo.