Jeuri ya Yanga inavyotunisha misuli

HAKUNA namna kwamba wale wapinzani wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, msimu ujao wana kazi kubwa ya kufanya ili kuwafanya wababe hao wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo wasitoboe katika mashindano ya ndani na hata yale ya kimataifa.

Ingawa kuna usajili unaoendelea katika viunga vya timu zote za ndani na zile za nje, lakini pale Jangwani kuna kila vaibu linalotikisa, linaloenda sambamba na usajili mpya, benchi jipya la ufundi pamoja aina ya mazoezi ambayo mastaa wa kikosi hicho washaanza kuyafanya.

Lakini, ikiwa ipo ukingoni kumalizia usajili wa kikosi kipya cha msimu ujao, Yanga kuna jeuri nyingine imeanza kuitengeneza nje ya uwanja ikitumia siku tano tu kutunisha msuli wa kifedha kwa dili mbili za maana zenye mabilioni ya shilingi.

Ndani ya siku hizo tano Yanga imekusanya jumla ya 25 Bilioni kupitia dili mbili tu za udhamini huku mmoja ya mabosi wa klabu hiyo akisema: “Subirini nyingine inakuja muda si mrefu.”

Ipo hivi. Agosti 7, Yanga ilisaini dili la kwanza la udhamini na kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya Haier yenye thamani ya Sh3.3 bilioni.

Udhamini huo ni kama Yanga iliuza eneo la bega moja tu la timu yao, eneo ambalo litatumika kuitangaza kampuni hiyo, iliyoongeza mkataba huo wa miaka mitatu.

Kama haitoshi juzi Jumatatu klabu hiyo ikaifunga siku hiyo kwa udhamini mwingine mzito wa Sh21.7 bilioni kutoka kwa kampuni nyingine kubwa ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa.

SportPesa itaendelea kuidhamini Yanga, ikiwa mdhamini mkuu wa mabingwa hao, ikiifanya ndoa yao na klabu hiyo kuendelea kwa miaka nane sasa tangu ilipoingia mara ya kwanza.

Awali, Julai 27, 2022 pande hizo mbili ziliingia mkataba wa miaka mitatu, uliokuwa na thamani ya sh 12.3 Bilioni, uliomalizika mwisho wa msimu uliopita.

Mkataba huo mpya ambao umesainiwa juzi umekuwa na ongezeko la Sh9.4 bilioni utakaoifanya  SportPesa kuendelea kukaa mbele ya jezi za mabingwa hao wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA) kwa misimu minne mfululizo.

SportPesa kwa mkataba huo utaifanya kujihakikishia umiliki wa eneo la mbele katika jezi za Yanga ambalo ndio lenye thamani kubwa, ikiacha wengine kugombea maeneo yaliyosalia.

Chini ya udhamini wa SportPesa, Yanga kwa misimu minne mfululizo imetawala soka la Tanzania kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la FA, Ligi ya Muungano na Ngao ya Jamii, lakini ikifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mbali na kucheza makundi ya Ligi ya Mabingwa na kufika robo fainali baada ya miaka 25 kupita tangu ilipofanya hivyo mwaka 1998.

Lakini, chini ya udhamini huo wa kishua, Yanga imeweza kufanya usajili wa wachezaji wenye majina makubwa sambamba na makocha walioifanya iwe moja ya timu inayoogopewa nchini na barani Afrika, kitu ambacho Rais wa klabu hiyo, Hersi Said alitamba katika hafla ya kusaini mkataba.

Hadi sasa Yanga imeshusha mashine mpya kukiimarisha kikosi hicho kutokana na nguvu ya kifedha, wakiwamo Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Balla Mousa Conte, Lassane Kouma, Celestin Ecua, Mohamed Doumbia, Andy Boyeli, AbdulNasir Mohammed ‘Casemiro’ na Abubakar Nizar ‘Ninju’.

“Mkataba wetu na Sportpesa umekuwa mkataba wenye manufaa makubwa kwa pande zote. Tunayo furaha kubwa kutangaza kuwa tumeongeza mkataba wetu na mdhamini wetu mkuu Sportpesa kwa kipindi cha miaka mitatu,” amesema Hersi alipozungumza katika hafla hiyo ya juzi.

“Tunaitumia fedha hizi za mkataba huu mpya, hizi ni fedha nyingi na niwahakikishe tutazitumia vizuri na kuhakikisha tunafanya Yanga inkuwa bora na bora zaidi.”

Hersi amesema mafanikio ya Stars kutinga robo fainali ya CHAN imechangiwa asilimia zote na wachezaji wanaocheza ndani ambao wanajengwa kutokana na fedha za udhamini wanaosapoti klabu na kuwepo kwa uongozi bora wa michezo na usimamizi mzuri ndio unaokuza soka la Tanzania.

Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa mkataba huo mpya, Mkurugenzi Mtendaji wa SportPesa, Tarimba Abbas alisema safari ya udhamini kwa Yanga ni kutokana na kuamini kwamba ni timu sahihi yenye mashabiki wengi na kwamba itaweza kubadili mpira wa Tanzania.

“Tumewahi kudhamini klabu nyingi kubwa zikiwemo Arsenal, Hull City, Everton na Ligi ya Kenya lakini hapa Tanzania tuliiona Yanga ndio klabu sahihi inayoweza kufanya nao kazi ili waubadilishe mpira wa Tanzania ,” alisema Tarimba na kuongeza:

“Tulipoingia Yanga tuliwapa nguvu ya kiuchumi, ndio maana mnaona sasa inaweza kumuuza mchezaji yeyote na ikanunua yeyote. Katika mkataba huu tumeweka kiwango kikubwa cha fedha ambacho kwa kuwa Yanga wanataka kushinda ubingwa wa Afrika basi kiasi hiki kitawafanya kupambana ili wakiupata watajipatia.”

Ofisa Mtendaji Mkuu wa zamani wa Yanga, Senzo Mazingiza akizungumzia dili hizo alisema hatua ya Haier na SportPesa kuendelea kuidhamini timu hiyo inakwenda kuchochea mafanikio kwa klabu hiyo.

“Kwanza niwapongeze viongozi wa Yanga, kuanzia Rais wa klabu rafiki yangu, Hersi (Said), Arafat (Haji) na Kamati ya Utendaji, kama kuna hatua muhimu ya kiungozi ni pale wadhamini wanapoamua kuongeza mkataba tena kwa thamani kubwa kama ambavyo imefanyika,” alisema Senzo na kuongeza:

“Hii inaonyesha kwamba taasisi hizo zina imani na uongozi na namna mambo yanaendeshwa lakini pia wadhamini nao wanaona fahari ya biashara zao kutangazwa na klabu yenye mafanikio.

“Unapozungumzia Bilioni 25, hiki ni kiasi kikubwa cha fedha kinachoenda kuchochea maendeleo makubwa kwa Yanga. Nimefanya kazi Yanga najua mahitaji ya kifedha ninachoweza kusema hizi fedha zitaongeza nguvu ya klabu hii kutamba Tanzania na nje ya Tanzania.

“Hatua kama hii ya kuendelea kusaini mikataba mikubwa ya udhamini ni kielelezo kwamba Yanga ilifanya mchakato mzuri wa mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu, ambayo sasa yanaendelea kuipa faida klabu hii kubwa.”