HATMA ya timu itakayoungana na Tanzania kutinga makundi ya michuano ya Ubingwa wa Nchi za Afrika (CHAN) 2024 kutoka Kundi B, inatarajiwa kujulikana leo Jumatano wakati mechi mbili tofauti zitakapopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Tanzania inayoongoza msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi tisa, tayari imeshakata tiketi ya kucheza robo fainali, huku timu tatu kati ya nne zilizosalia zikiifukuzia nafasi moja iliyosalia na mechi za leo ndizo zinazoweza kutoa ramani ya ipi inayoweza kuungana na Taifa Stars.
Mapema saa 11:00 jioni, Madagascar iliyotoka kupasuka mbele ya Tanzania katika mechi iliyopita itakuwa wenyeji wa Afrika ya Kati inayoburuza mkia wa kundi hilo baada ya kupoteza michezo miwili ya awali, lakini ikiwa na uwezo wa kufikisha alama sita kama itashinda mechi zilizosalia.
Baada ya shughuli hiyo, Saa 2:00 usiku itakuwa ni zamu ya Mauritania iliyotoka kushinda mechi iliypoita dhidi ya Afrika ya Kati itapepetana na Burkina Faso, iliyo na pointi tatu kutokana na kushinda mechi iliyopita pia dhidi ya Afrika ya Kati.
Mauritania mechi ya leo itakuwa ni ya kufungia kundi na kama itashinda itafikisha pointi saba kwani kwa sasa ina nne ikishika nafasi ya pili, juu ya Madagascar itakayokuwa ikifikisha mechi ya tatu sawa na Afrika ya Kati na Burkina Faso.
Kimahesabu mechi zote za leo zina umuhimu kwa kila timu, lakini Mauritania inahitaji ushindi kwani itakamilisha idadi ya mechi nne na kufunga hesabu, ilihali timu tatu zilizosalia zitakuwa zikifikisha mechi tatu na kusaliwa na moja kama ilivyo kwa Tanzania.
Mechi ya jioni ni muhimu pia kwa Afrika ya Kati kwani ikipoteza itakuwa ya kwanza kuaga fainali hizo, lakini ina kibarua kigumu mbele ya Madagascar iliyoonyesha soka tamu mechi mbili zilizopita, ilipotoka sare mbele ya Mauritania licha ya kuwa pungufu na ilipopoteza kwa Tanzania 2-1.
Hili litakuwa ni pambano la nane kwa Afrika ya Kati na Madagascar kukutana katika mashindano, huku Madagascar ikiwa na rekodi ya kushinda mara tatu dhidi ya mbili za wapinzani wao zilipokutana katika mechi za kuwania Fainali za Kombe la Dunia na hata Afcon kwa mara kadhaa.
Mechi mbili pekee baina yao zilizoisha kwa sare, kuonyesha ni timu zinazojuana na leo zitakuwa na kazi na kuthibitisha ubora na Machi mwaka huu zilipokutana katika mechi za kuwania fainali za Kombe la Dunia Madagascar ikiwa ugenini iliishindilia Afrika ya Kati mabao 4-1.
Timu zote zina sifa za kucheza kwa kasi, japo mashambulizi yao kuanza taratibu kuanzia nyuma, pi zotye zina udhaifu wa kujilinda, Afrika ya Kati ikiwa imeruhusu mabao matano katika mechi mbili, huku Madagascar ni mechi moja tu iliyocheza bila kuruhusu bao, lakini iliyofuata iliruhusu mawili.
Kwa mechi ya usiku kazi itakuwa kubwa zaidi kwa vile timu zote mbili zina nafasi ya kujiweka pazuri kuifuata Tanzania, Mauritania ina pointi nne, ikiwa ni moja zaidi ya Burkina Faso ambayo imekuwa na uwezo wa kufunga, lakini ikiwa na ukuta mwepesi ikiifukuzia Afrika ya Kati.
Timu hiyo ya Burkina faso imefunga mabao manne na kufungwa manne na imekuwa ikicheza soka tamu la kushambulia kwa pamoja kwa kasi ndio maana imetengeneza penalti tatu katika mechi mbili zilizopita, ikifungwa moja na yenyewe kufunga mbili.
Timu hizo zimeshakutana mara 10 katika mechi tofauti zikiwemo za kirafiki na za kimashindano tangu mwaka 1976 hadi mwaka jana, huku Burkina Faso ikishinda mara tano dhidi ya moja ya wapinzani wao na zilizosalia zimeisha kwa sare.
Hata hivyo kwa aina ya uchezaji wa timu zote, huenda leo mashabiki watakaoenda uwanjani na wale watakofuatilia kupitia runinga wakashuhudia burudani yenye mabao mengi na timu yote ina nafasi ya kuibuka na ushindi, japo inategemea zaidi na itakavyoshuka uwanjani kimbinu dhidi ya mpinzani.
Kundi hilo litamaliza mechi zao wikiendi hii, wakati Tanzania itakamilisha ratiba dhidi ya Afrika ya Kati na Burkina Faso kupepetana na Madagascar na kujua nani anamaliza nafasi ya pili ili kucheza na washindi wawili wa Kundi A linalocheza mechi zake jijini Nairobi Kenya.
Mechi hizo za robo zimepangwa kuanza Agosti 22, ambapo Tanzania itavaana na mshindi wa pili wa Kundi A saa 11:00 jioni, kabla ya kufuatiwa na mechi ya mshindi wa kwanza wa Kundi D ambalo mechi zake zinapigwa visiwani Zanzibar dhidi ya mshindi wa pili wa Kundi C lililopo, Uganda.Keshokutwa Alhamisi.