MASHABIKI wanaohudhuria mechi mbalimbali za mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN 2024 wametakiwa kuzingatia miongozo ya usalama na ulinzi iliyotolewa na Kamati ya Maandalizi (LOC) pamoja na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ili kuepuka adhabu na usumbufu.
LOC imeweka bayana mabango, bendera au alama zenye ujumbe wa kisiasa, dini, kibaguzi au wa kuchochea chuki kati ya makundi mbalimbali hayaruhusiwi kuingizwa viwanjani. Hatua hii inalenga kulinda hadhi ya mashindano na kuhakikisha viwanja vinabaki kuwa sehemu ya amani na mshikamano wa michezo.
Mabango pekee yatakayoruhusiwa ni yale yenye ujumbe wa kuunga mkono timu au wachezaji bila mwelekeo wa kisiasa. Kwa mashabiki wanaotaka kuingia na mabango, miongozo imeweka wazi ni lazima kwanza kutuma ombi rasmi kwa CAF kupitia barua pepe, ili ujumbe na muundo wa bango uhakikiwe na kuidhinishwa kabla ya kuingia uwanjani.
Kwa mujibu wa taarifa za LOC, taratibu hizi zimewekwa baada ya CAF kushuhudia mara kadhaa mashindano makubwa yakigeuzwa majukwaa ya matamko ya kisiasa, jambo linalopingana na kanuni zake za maadili na usalama.
Aidha, mashabiki wametahadharishwa kuwa kuvaa jezi au vifaa vya michezo vyenye nembo za kampuni ambazo si sehemu ya orodha ya wadhamini wa mashindano kunaweza kukiuka masharti ya udhamini, ikizingatiwa michuano ya CHAN inafadhiliwa na kampuni yaliyowekeza fedha nyingi kwa maandalizi, matangazo na zawadi.
Orodha ya vifaa vilivyopigwa marufuku kuingia viwanjani inajumuisha filimbi, fataki, silaha za aina yoyote, chupa za kioo na vifaa vya muziki vyenye kelele kubwa. Hatua hizi zimekusudiwa kulinda usalama wa mashabiki, kuzuia vurugu na kuhakikisha wachezaji wanacheza bila usumbufu.
Katika utekelezaji wa kanuni hizo, CAF kupitia Bodi ya Nidhamu imeitoza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) faini ya Dola 10,000 (zaidi ya Sh25milioni) baada ya kubainika kuvunja masharti ya usalama na ulinzi yaliyobainishwa katika Ibara ya 82 na 83 za kanuni za nidhamu za CAF pamoja na Ibara ya 24 na 28 za kanuni za Usalama na Ulinzi za CAF.
Adhabu hiyo inatokana na vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyofanywa na mashabiki wakati wa mechi ya Tanzania dhidi ya Burkina Faso katika CHAN 2024.
Kwa mujibu wa Ibara ya 82 ya kanuni za nidhamu za CAF, mashirikisho ya kitaifa yanawajibika kwa vitendo vya mashabiki wao, ikiwa ni pamoja na vurugu, utovu wa nidhamu au uharibifu wa mali, hata kama havikufanywa na viongozi au wachezaji moja kwa moja. Ibara ya 83 inasisitiza uvunjaji wa masharti ya usalama unaweza kupelekea faini, kuzuiwa kuingia viwanjani, au adhabu nyingine kulingana na ukubwa wa kosa.