Lissu alivyojipanga kutema nyongo leo kesi ya uhaini

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini leo tena Jumatano, Agosti 13, 2025
anapanda kizimbani, katika hatua ambayo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) anatarajiwa kuweka wazi ushahidi atakaoutumia kwenye kesi hiyo, kama ataipeleka Mahakama Kuu.

Kwa upande wake, Lissu anatarajiwa kuanza kujibu mapigo kwa kutema nyongo kupitia maelezo yake marefu ya utetezi wake aliyokwisha kuyaandaa, ambayo ameshaweka wazi kuwa anayawasilisha katika hatua hiyo kabla ya kwenda Mahakama Kuu ambako ndiko atakakosikilizwa.

Lissu anakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, ililofunguliwa kwa ajili ya uchunguzi wa awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu itakakosikilizwa katika hatua ya ushahidi na kuamuliwa.

Leo Jumatano, kesi hiyo  imepangwa pamoja na mambo mengine kwa ajili ya mwenendo kabidhi yaani kuihamisha kwenda Mahakama Kuu (committal proceedings), kama  Mkurugenzi wa Mashtaka atakuwa ameshapeleka hati ya mashtaka Mahakama Kuu.

Utaratibu na hatua muhimu

Kesi za makosa makubwa likiwemo la uhaini husikilizwa na kuamuliwa na  Mahakama Kuu.

Hata hivyo, hufunguliwa kwanza katika Mahakama za chini, Mahakama za wilaya au Mahakama za Hakimu Mkazi kwa ajili  ya uchunguzi wa awali ikiwemo kukamilisha upelelezi kwa maandalizi ya kwenda kusikilizwa Mahakama Kuu.

Baada ya hatua hizo hasa, upelelezi kukamilika DPP hupeleka hati ya mashtaka Mahakama Kuu ambako husajiliwa.

Kisha DPP anaiarifu Mahakama ya chini kuhusu hatua hiyo, hivyo Mahakama hiyo ya chini inangia katika hatua ya  mwenendo kabidhi (wa uhamishwaji kwenda Mahakama).

Katika hatua hiyo mshtakiwa husomewa hati ya mashtaka iliyopelekwa na kusajiliwa Mahakama Kuu, kisha anasomewa maelezo ya ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka wanaotarajiwa kuitwa mahakamani kutoa ushahidi pamoja na vielelezo vitakavyotumika.

Kisha mahakama  itampa nafasi kama ana jambo lolote la kusema baada ya kumfahamisha wazi kuwa ana haki ya kuutunza utetezi wake au kusema jambo lolote muhimu na kila atakachokisema Mahakama italiandika kama kilivyo na kitatumika kama ushahidi katika kesi yake.

Washtakiwa wengi katika hatua hiyo wanapopewa nafasi huwa hawasemi chochote kuhusiana na kiini cha kesi isipokuwa malalamiko, changamoto wanazokumbana nazo mahabusu.

Hata hivyo, hili kwa Lissu leo linatarajiwa kuwa tofauti, kwani amejipanga kikamilifu kutumia hiyo fursa hiyo kutema nyongo yake.

Mara ya mwisho kesi hiyo ilipotajwa Julai 30, 2025 Lissu aliieleza Mahakama  ameandaa maelezo yake ya maandishi kurasa 101, ambayo alitarajia kuyatoa siku hiyo, kama taratibu zingekuwa zimekamilika.

Kwa wingi huo wa maelezo hayo ni dhahiri Lissu amejiandaa kutema nyongo ya moyoni, kwa kuweka wazi utetezi wake, mapema kabisa hata kabla ya wakati wa usikilizwaji kamili wa kesi hiyo.

Julai 15, 2025 upande wa mashtaka uliiarifu mahakama hiyo kuwa tayari upelelezi umeshakamilika na kwamba DPP ameridhika na ushahidi kuwa unatosha  kupeleka kesi hiyo Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji.

Hata hivyo, kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka wa kesi hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga aliieleza mahakama hiyo ya chini kuwa DPP alikuwa hajapeleka hati ya mashtaka Mahakama Kuu.

Alidai  hatua hiyo ilikuwa haijafanyika  kwa kuwa walikuwa wamefungua shauri dogo Mahakama Kuu.

Wakili Katuga alieleza katika shauri hilo la maombi ya jinai namba 17059 ya mwaka 2025 wanaomba amri ya ulinzi wa baadhi ya mashahidi katika kesi hiyo, yaani kutokuwekwa wazi kwa taarifa zao zinaweza kufanya utambulisho wao kubainika.

Alifafanua shauri hilo limefunguliwa chini ya kifungu cha 194 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Marejeo ya mwaka 2023, kinaruhusu kuwasilishwa maombi ya ulinzi wa taarifa za mashahidi kwa ajili ya usalama wao.

Hivyo Wakili Katuga, chini ya kifungu cha 265 cha CPA aliiomba ahirisho kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa maombi hayo, kabla ya kupeleka kesi hiyo Mahakama Kuu.

Lissu ambaye katika kesi hiyo anajitetea mwenyewe, alipinga vikali maombi ya Jamhuri ya ahirisho, akidai kilichotakiwa siku hiyo chini ya kifungu cha 262 (6) cha CPA ni kuiarifu Mahakama hiyo kuwa taarifa ya kesi hiyo  imeshapelekwa Mahakama Kuu (kusajili kesi).

Alidai masharti ya  kifungu hicho hayakuzingatiwa na upande wa mashtaka.

Hivyo aliiomba mahakama kwa kutumia mamlaka yake kukataa kutoa ahirisho, badala yake iamuru kumfutia mashtaka kuamuru aachiliwe huru.

Hata hivyo, Hakimu Mafawidhi wa Mahakama hiyo anayesikili kesi hiyo katika hatua hiyo ya awali, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga alikataa hoja na maombi ya Lissu.

Alieleza upande wa mashtaka ulikuwa sahihi kisheria.

Hivyo aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 30, 2025 kwa ajili ya kuangalia kama upande wa mashtaka utakuwa umeshasajili kesi hiyo Mahakama Kuu, ili mahakama hiyo iweze kuendelea na hatua ya mwenendo kabidhi.

Julai 30, Wakili Katuga aliiarifu Mahakama bado hati ya mashtaka ilikuwa haijapelekwa Mahakama Kuu kwani bado shauri hilo dogo lilikuwa halijaamuliwa na kwamba lilikuwa limepangwa kuamuliwa Agosti 4, 2025.

Hivyo aliomba mahakama hiyo itoe amri ya ahirisho na kupanga tarehe nyingine kusubiri uamuzi huo wa Mahakama Kuu katika shauri hilo.

Kwa mara nyingine Lissu alipinga vikali maombi ya Jamhuri ya ahirisho akidai ilishindwa kutekeleza amri ya Mahakama kwa kutokuwasilisha Mahakama Kuu hayo ya mashtaka ili kuiwezesha kufanyika mwenendo kabidhi siku hiyo.

Hivyo aliomba mahakama isikubali kutoa ahirisho badala yake iamuru Jamhuri waendelee na mwenendo kabidhi au iamuru aachiliwe huru.

Hakimu Kiswaga aliahirisha kesi hiyo mpaka leo Jumatano kwanza, kwa ajili ya uamuzi wa pingamizi la Lissu kukataa ahirisho au kumwachilia huru.

Pia Hakimu Kiswaga alielekeza upande wa mashtaka kufuatia uamuzi wa shauri hilo ili kuhakikisha wanapeleka hati ya mashtaka Mahakama Kuu kuiwezesha kuendelea na mwenendo kabidhi leo.

Agosti 4, 2025, Mahakama Kuu ilitoa uamuzi wa shauri hilo la Jamhuri kuwalinda mashahidi wake, ambalo iliridhia maombi ya Jamhuri na kutoa amri zilizoombwa.

Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kutenda kosa hili Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam.

Anadaiwa kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.

Endelea kufuatilia Mwananchi