Maisha ya binadamu ni hadithi. Matendo ya uhai ni wino. Kadiri unavyoishi ndivyo unavyoandika simulizi yako. Idadi ya kurasa, hutegemea umri, vilevile wingi wa matendo. Wapo walioishi umri mdogo, wakajaza kurasa mamia, vivyo hivyo kinyume chake.
Job Yustino Ndugai, kuanzia kuzaliwa kwake, Januari 21, 1963 mpaka alipokata kauli, Agosti 6, 2025, ni miaka 62, miezi sita na siku 16. Hesabu hiyo ukiigawa kwa saa 24, unapata siku 22,827. Hivyo, uhai wa Ndugai kama wino, andiko lake lilikamilika ndani ya siku 22,827.
Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, alipata kusema: “Maisha ya binadamu ni hadithi tu hapa ulimwenguni. Basi, eeh ndugu yangu, kuwa hadithi nzuri kwa hao watakaosimuliwa.” Mwisho wa kunukuu.
Ukishavuta pumzi ya mwisho, inakuwa mwisho wa wino wako. Hutaandika tena. Kitakachobaki ni simulizi. Je, ulikuwa mwema kiasi gani? Uovu wako utadhihirika? Waliobaki nyuma yako watasimuliana.
Hata sasa, Ndugai akiwa amelala nyumbani kwake, ndani ya shamba lake, lililopo kijiji cha Madumbwa, wilayani Kongwa, Dodoma, hana ambacho anaweza kusimulia kuongeza utamu au uchungu wa hadithi yake, isipokuwa yale alitoyatenda ndani ya siku 22,827.
Yote yanaweza kusemwa kuhusu Ndugai, lakini huwezi kumtenganisha na Kongwa yake. Aliipenda, aliitumikia, aliivaa kama beji ya heshima, aliishi Kongwa na amezikwa wilayani humo, ndani ya jimbo aliloliwakilisha bungeni kwa miaka 25.
Alizaliwa Kijiji cha Raikala, Kata ya Sagara, Kongwa. Aliizunguka nchi na dunia katika msako wa elimu na maisha kwa jumla, lakini siku zote alihakikisha Kongwa panabaki makao makuu yake. Kongwa ni mahali ambapo Ndugai alipaita nyumbani.
Alisoma Shule ya Msingi Mahambe, Ikungi, Singida, mwaka 1971 mpaka 1977. Alipata ufaulu mkubwa na kuchaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza mpaka cha nne, Shule ya Sekondari Kibaha, Pwani, mwaka 1978 hadi 1981. Kisha, kidato cha tano na sita, Shule ya Juu ya Old Moshi, Kilimanjaro, mwaka 1982 na kuhitimu 1984.
Mtaalamu wa wanyamapori, aliyetunukiwa stashahada ya Usimamizi wa Wanyamapori, Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka, mwaka 1988. Ndugai ni mwanasayansi. Kati ya mwaka 1990 na 1993, alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na kutunukiwa Shahada ya Sayansi ya Ikolojia na Zolojia.
Mwaka 1995, alihitimu Stashahada ya Umahiri (postgraduate diploma), katika usimamizi wa Maliasili na Kilimo Endelevu, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Norway. Baada ya hapo, aliendelea na Shahada ya Uzamili ya usimamizi wa Maliasili na Kilimo Endelevu, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Norway.
Ndugai, pia ana Shahada ya Uongozi, aliyoipata Shule ya Uongozi ya Maastricht ya Uholanzi, kupitia mradi wa pamoja na Taasisi ya Uongozi ya Mashariki na Kusini ya Afrika (Esami). Hapa hakuna ubishi kuwa wino wa msako wa elimu, Ndugai ameacha simulizi bora.
Ndugai alianza ajira kama ofisa msaidizi wa wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii. Alipanda ngazi hadi meneja mradi, ukanda wa Mashariki, Hifadhi ya Selous, kisha Mkurugenzi wa Mradi wa Uhifadhi wa Kanda ya Serengeti, hadi mwaka 2000, alipojitosa kugombea ubunge na kushinda.
Hili la ajira nalo wino wake upo barabara. Ndugai aliingia kazini kama ofisa wa chini, akapanda mpaka kuwa mkurugenzi. Huwezi kupanda ngazi kazini bila kuonesha jitihada na utofauti. Ndugai alidhihirisha utofauti kazini.
Hata bungeni, Ndugai alipoingia mwaka 2000, moja kwa moja alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mazingira, Maliasili na Utalii. Mwaka 2005 hadi 2010, Ndugai alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira, Maliasili na Utalii, vilevile Mwenyekiti wa vikao vya Bunge.
Mwaka 2010 mpaka 2015, Ndugai alikuwa Naibu Spika, halafu Novemba 2015 mpaka Januari 2022, Ndugai alikuwa Spika wa Bunge. Hili pia linadhihirisha kuwa hadithi ya Ndugai ipo bayana kuhusu mwenendo aliokuwa nao wa kupanda ngazi kutoka chini, kila alipoingia kazini.
Siku 22,827 za maisha ya Ndugai duniani, zina nyakati nyingi za furaha, mafanikio yake katika msako wa elimu na matokeo makubwa ya kupanda ngazi kutoka chini hadi kuwa kiongozi mkuu wa mhimili wa kutunga sheria, Bunge.
Hata hivyo, katika siku hizo, yapo maeneo wino haujaacha andiko zuri kuhusu Ndugai. Ni jinsi alivyoendesha Bunge, kipindi chote akiwa Spika. Kila wasifu wa Ndugai utakapotajwa kuhusu namna alivyoliongoza Bunge, hadithi ya mhimili huo kukosa meno dhidi ya Serikali itaibuka.
Ndugai, jinsi alivyochagua kupambana na wapinzani, badala ya kuongoza Bunge kwa usawa, ni wino ambao umeandika hadithi yake katika siku zake za uhai, 22,827. Msimamo wa kambi ya chama chake (CCM), ulimmeza, akawa rungu kwa wapinzani.
Bunge la Ndugai lilichora mstari wa kuikwepa Serikali. Rais wa Tanzania akiwa Dk John Magufuli, ilionekana waziwazi Bunge lilipokea maagizo ya Serikali. Magufuli alimwambia Ndugai awafukuze wabunge wa upinzani bungeni, ili wangezungumza nje Bunge, angewashughulikia, kwani wasingekuwa na kinga. Ndugai aliwatimua kweli.
Hadi mpangilio wa kamati teule za Bunge, Ndugai alishauriana na Rais Magufuli, hivyo kutia doa dhana ya uwepo wa mihimili mitatu, ambayo kila mmoja unajitegemea. Ndugai aliunda kamati teule ya kuichunguza Serikali, lakini alifanya mashauriano na Mkuu wa Serikali, Dk Magufuli.
Wino umeshaandika na haitafutika kuwa Ndugai ndiye aliyewaapisha wabunge 19 wa viti maalum, Chadema, bila ridhaa ya uongozi wa chama hicho. Na aliwakingia kifua hata vikao halali Chadema, vilipoamua kuwavua uanachama wabunge hao.
Ndugai alipenda utani. Zama zake akiwa Spika wa Bunge, alipenda kuachia mijadala ya uchokozi ili kuchangamsha vikao. Ndugai pia, alipenda mawazo tofauti, ndiyo maana alimwita profesa, Mbunge wa Kahama Mjini, Jumanne Kishimba.
Hesabu ya jumla, Ndugai ni binadamu. Hivyo hadithi yake haiwezi kuwa nyeupe na furaha peke yake kama malaika. Zipo nyakati za maumivu, kama ambavyo alituhumiwa kwa kuonekana alikosa ubinadamu kumfuta ubunge, Tundu Lissu, aliyekuwa akitibiwa nje ya nchi, baada ya kupigwa risasi.
Hadithi ya binadamu ni kurasa za rangi tofauti; nyeusi kama msiba, bluu majonzi, nyekundu inaweza kuwa damu au upendo, ndivyo kwa Ndugai; yapo maeneo alipendwa sana, kwingine walimchukia. Muhimu, wino wake umeshaandika, na kwa mantiki hiyo, hatasahaulika.