WALIMU WA NGUMI 30 KUTOKA TANZANIA WAMALIZA MAFUNZO YA KIMATAIFA

Pichani wa kwanza kushoto ni mkufunzi Dr. Gabriel Martelli, picha ya pili ni baadhi ya walimu washiriki wa mafunzo ya kimataifa na viongozi wa BFT walioshiriki katika darasa la pamoja lililofanyika Dar es salaam.
*Malawi, Ethiopia, Comoros, Bangladesh pia washiriki.
JUMLA ya Walimu wa mchezo wa ngumi 36 kutoka mataifa ya Tanzania (30), Ethiopia (3), Malawi (1), Comoros (1) na Bangladesh (1) wamefanikiwa kumaliza mafunzo ya Kimataifa ya Ualimu ya Nyota 1 yaliyofanyika kuanzia tarehe 26-07-2025 mpaka tarehe 06-08-2025.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), yaliendeshwa na mkufunzi mkuu wa Chama Cha Ngumi cha Dunia na Chama Ngumi cha Ulaya Dr. Gabriel Martelli kwa njia ya mtandao na darasa maalumu katika jengo la CCM kata ya Manzese, Jijini Dar es salaam.
“Ni hatua kubwa na yakujivunia katika mipango yetu BFT kuleta maendeleo na mapinduzi katika mchezo wa ngumi hasa kwa kuwezesha mafunzo ya Kimataifa kwa walimu wetu nchini, tutaandaa mafunzo mengi zaidi ili kuongeza wigo kwa wanufaika. Tunamshukuru Mungu kwa kila hatua, tunaendelea kutekeleza kwa vitendo” alinukuliwa Rais wa BFT Ndg. Lukelo Willilo.
Walimu walionufaika katika mafunzo haya walitokea katika mikoa ya Dar es salaam, Pwani, Kagera na Mwanza pamoja na vyombo vya Ulinzi na Usalama vya JWTZ, JKT, Polisi na Magereza.
Shirikisho linatarajia kuendesha mafunzo mengine ya walimu ya kimataifa hapo badae mwaka huu nchini Tanzania kwa kulenga walimu 50 kuweza kunufaika.