Kwa kawaida kipindi cha uchaguzi huonekana kama fursa ya wananchi kuamua kina nani wataongoza nchi na kuwa wawakilishi wao katika vyombo vya kutunga sheria na mabaraza ya utawala.
Hata hivyo, hali ni tofauti kwa Zanzibar, ambako kila unapokaribia uchaguzi na baada ya kutangazwa matokeo, hewa ya wasiwasi na taharuki hutanda.
Sababu kuu ya hali hii ni changamoto mbalimbali, zikiwamo ukosefu wa uhakika wa mahali kura zitahesabiwa na vizuizi vinavyowekwa kwa waandishi wa habari.
Mara nyingi waandishi huzuia kutangaza matokeo yaliyo wazi na yamebandikwa kwenye vituo au kuhoji matukio yanayokiuka sheria na taratibu, jambo linalokumbwa na upinzani na bughudha.
Historia inaonyesha katika chaguzi zilizopita, vitendo vya vurugu, kupigwa na hata mauaji vilianza kutokea miezi kadhaa kabla na kuendelea hata baada ya uchaguzi.
Kinachotia uchungu ni kwamba matukio haya ambayo mara nyingine yana sifa za uhalifu wa wazi, hufunikwa kwa kauli kwamba “hali ni shwari” na kwamba “amani imetawala.” Lakini amani haiwezi kumaanisha kuwapo vitisho, watu kutandikwa, au kuuawa.
Ingawa viongozi na taasisi mbalimbali wamekuwa wakitoa kauli za kutuliza na kuwahakikishia wananchi kuwapo kwa amani, dalili za vitisho tayari zimeanza kuonekana.
Mfano ni malalamiko ya wafanyakazi wa serikali kulazimishwa kupeleka kadi zao za kupiga kura ofisini kwa kisingizio cha “kuratibiwa,” kitendo ambacho kinakiuka haki za msingi za wapigakura.
Cha kushangaza, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), yenye jukumu la kuhakikisha uchaguzi unafuata sheria, imekaa kimya licha ya ushahidi wa vitendo hivi.
Hata malalamiko ya hivi karibuni kuhusu watu kupigwa, kuporwa fedha, mali na hata kadi za kura hayajashughulikiwa.
Askari wa manispaa wamekuwa wakionekana waziwazi wakitisha wananchi, kuwapiga na kuwapora, huku mamlaka zinazowaajiri zikipuuzia malalamiko hayo na mara nyingine hata kuwalinda.
Kadri tunavyokaribia kuanza rasmi kampeni, hali hii inazua mashaka makubwa kuhusu siku yenyewe ya kupiga kura.
Ikiwa vikundi vya vijana wanaovaa “ninja” vitaendelea kutembea mitaani na majumbani kupiga na hata kuua watu kama ilivyowahi kutokea, basi hatuwezi kutarajia amani.
Upo ushahidi wa video, picha, vyeti vya matibabu, na orodha ya waliopoteza maisha au kujeruhiwa, waliogeuka vilema, wajane na mayatima kutokana na vurugu za kisiasa. Ni dhahiri kuwa Jeshi la Polisi, kama mlinzi mkuu wa usalama wa raia na mali zao, linapaswa kuchukua hatua kali kudhibiti makundi haya.
Vikosi vingine vya ulinzi na usalama havipaswi kuchukua majukumu ya polisi, na askari wa manispaa lazima wawekwe chini ya udhibiti mkali, kwani wengi wao hawana hata mafunzo ya msingi kuhusu haki za raia.
Historia inatufundisha kuwa watu wakihisi kunyanyaswa na kudhulumiwa huweza kupoteza subira na kulipiza kisasi, hali ambayo inaweza kuchochea machafuko.
Ili kuepuka hali hiyo, ni lazima kuacha vitendo vya kutumia nguvu dhidi ya raia, ikiwamo kupiga, kupora mali na kadi za kura. Hatua ya kwanza ni kuwabaini na kuwachukulia hatua wote wanaokiuka sheria na wale wanaotoa amri hizo.
Kuna taarifa za uwepo wa vituo vya mateso, ikiwamo chumba kinachodaiwa kuwa katika Ofisi ya Mji Mkongwe na eneo la Buyu, nje ya mji wa Unguja.
Taarifa hizi hazipaswi kupuuzwa; zinahitaji uchunguzi wa kina wa polisi au tume maalumu. Kama hazina ukweli, walalamikaji wawajibishwe kisheria kwa kutoa taarifa za uongo.
Lakini kupuuzia ushahidi wa video unaoonyesha watu wakipigwa si hatua ya busara. Ni vigumu kuamini kwamba video hizo zote ni za kubuni.
Wazanzibari wanapaswa kujiuliza: je, ni lazima watu kuumizwa kimwili na kiakili kila uchaguzi unapokaribia?
Na kwa nini kadi ya kupiga kura isiwe mali halali ya mpigakura aliyesajiliwa, badala ya kuwekwa mikononi mwa mamlaka au waajiri?
Kila mara tunasikia kauli kwamba Wazanzibari ni ndugu, wanapendana na kuheshimiana. Lakini upendo na heshima haviwezi kudhihirishwa kwa kupigana, kudhulumu au kuumizana.
Ni wakati sasa wa kuhakikisha matamshi ya kutaka amani na mshikamano yanaambatana na vitendo halisi.
Hili litawezekana tu ikiwa kila mtu ataheshimu sheria za nchi na yeyote atakayezivunja awajibishwe bila kujali cheo, nafasi au undugu wake.
Uchaguzi huru na wa amani Zanzibar unawezekana, lakini unahitaji ujasiri wa kulinda utu wa kila mwananchi.