Serikali kuvuna Sh719 bilioni mikataba ya uwekezaji sekta ya utalii

Dar es Salaam. Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) imesaini mikataba minne ya uwekezaji wa utalii kupitia utaratibu wa Uwekezaji Mahiri (Swica) na kampuni ya Kitanzania ya Uhusiano International ICT Ltd.

Mikataba hiyo inatarajiwa kuingiza mapato ya Dola za Marekani milioni 281.5 (sawa na Sh719 bilioni za Kitanzania) kwa kipindi cha miaka 20 ikiwa ni wastani wa Sh36 bilioni kwa mwaka, imesainiwa leo Jumatano Agosti 13, 2025.

Hafla ya utiaji saini imefanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam na imehusu uwekezaji katika vitalu vinne vya Burko Open Area (Monduli – Arusha), Selous MHJ1, Selous MHJ2 na Selous ML1 (Liwale – Lindi), vyote vikiwa chini ya Kampuni ya Uhusiano International ICT Ltd inayomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana amesema uwekezaji huo utaimarisha sekta ya uwindaji wa kitalii na utalii wa picha, sambamba na kuleta ajira, kuboresha huduma za jamii na kuchochea maendeleo ya wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya uwekezaji. Miradi ya maendeleo itakayoibuliwa na wananchi wenyewe inakadiriwa kugharimu Dola milioni 1.8 (sawa na Sh4.6 bilioni) kwa miaka 20.

Balozi Dk Chana pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake madhubuti katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia filamu za Amazing Tanzania na The Royal Tour, zilizochochea ongezeko la watalii na wawekezaji.

Ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kusisitiza umuhimu wa matumizi endelevu ya rasilimali kwa kuzingatia sheria, kanuni na misingi ya uhifadhi bora. Alitoa wito kwa wawekezaji zaidi kuja kuwekeza katika vivutio vya kipekee vya utalii vilivyopo nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tawa, Meja Jenerali mstaafu, Hamis Semfuko amesema Tawa imepiga hatua kwa kusaini mikataba minne mipya ya Swica na kufikisha jumla ya mikataba 13 kati ya 14 iliyopangwa sawa na asilimia 92.3 ya lengo, hatua iliyowezesha kukusanya zaidi ya Sh27.4 bilioni kati ya Januari 2024 na Agosti 2025.

Aidha, Meja Jenerali Semfuko amebainisha kuwa Tawa ipo katika hatua za mwisho kusaini mkataba na Kampuni ya GBP Trading Ltd (GTL) kwa ajili ya ujenzi wa kambi za kudumu za kitalii katika hifadhi za Kijereshi, Mpanga-Kipengere na Wami-Mbiki, hatua itakayoongeza vitanda 240 na kupunguza uhaba wa malazi kwa watalii.

Awali, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Tawa, Mlage Kabange, amesema tangu kusainiwa kwa mikataba ya awali ya SWICA mwaka 2024, Tawa imeshuhudia ongezeko la mapato  kutoka Sh55 bilioni hadi Sh87.12 bilioni katika mwaka wa fedha 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 158.2.

Aliongeza kuwa Tawa inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji, ikiwemo ujenzi wa kilomita 453.2 za barabara kwa kiwango cha changarawe katika maeneo ya kimkakati sawa na asilimia 40 ya lengo la kujenga kilomita 1,127 ifikapo mwaka 2026.

Kamishna Kabange amesisitiza kuwa Tawa ipo tayari kushirikiana na wawekezaji ili kuhakikisha utekelezaji bora wa mikataba hiyo kwa manufaa ya Taifa na wananchi.

Mwenyekiti wa Kampuni ya Uhusiano International ICT Ltd, Zahir Mulla ametoa shukrani kwa Rais Samia, Wizara ya Maliasili na Utalii, pamoja na Bodi na Menejimenti ya Tawa kwa kuridhia pendekezo lao la uwekezaji. Amesema huu ni mwanzo mzuri kwa wawekezaji wa ndani kuonesha uwezo wao katika sekta ya utalii.