Tani 30 za dawa za kulevya kwa jina la mbolea zanaswa

Dar es Salaam. Tani 18.5 za shehena ya dawa mpya za kulevya aina ya Mitragyna Speciosa zimekamatwa zikiwa zimeingizwa nchini Tanzania kama mbolea kwa ajili ya bustani za mbogamboga na maua.

Dawa hizo, zilizokuwa zimefungashwa kwenye mifuko 756 ndani ya kontena la futi 40, ziliingizwa Tanzania kwa ajili ya kufungashwa upya na kutafutiwa soko la ndani na nje ya nchi.

Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara, shehena hiyo ilibainika si mbolea bali ni dawa za kulevya.

Hii si mara ya kwanza kwa aina hiyo mpya ya dawa za kulevya kukamatwa Tanzania, kwani Juni 2025 kontena lenye futi 40 lilikamatwa likiwa na shehena ya tani 11.5 ya dawa hizo zikiwa zimefungashwa kwenye mifuko 450 kwa jina la mbolea.

Shehena hiyo ya dawa za kulevya iliingia nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam ikiwa na nyaraka zote zinazoonesha ni mbolea na ikatolewa hadi kwenye eneo ilipohifadhiwa kabla ya kukamatwa.

Akizungumza leo Jumatano, Agosti 13, 2025 jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, amesema watuhumiwa saba wamekamatwa wakihusishwa na dawa hizo, wakiwemo raia wawili wa Sri Lanka na Watanzania watano.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo akizungumzia kukamatwa kwa shehena ya dawa za kulevya zilizoingizwa nchini kama mbolea.

Amesema watuhumiwa hao ndiyo waliohusika katika uingizwaji wa shehena iliyokamatwa Juni 2025 na wamefanya hivyo katika nchi kadhaa bila kukamatwa.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema ukamataji wa Mitragyna Speciosa ni ishara ya kuwepo kwa changamoto mpya katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini.

“Hivyo, tutaendelea kuimarisha ufuatiliaji na udhibiti zaidi wa biashara ya dawa hii pamoja na dawa nyingine za kulevya hapa nchini. Hawa waliingiza mzigo huu kwa harakaharaka wakiamini tutakuwa bize kushughulika na ile tuliyoikamata,” amesema.

Mitragyna Speciosa ni aina mpya ya dawa za kulevya inayotokana na mmea unaofahamika kwa jina la Kratom, ambao hupatikana zaidi katika nchi za Kusini Mashariki mwa Bara la Asia.

Dawa hiyo inatajwa kuwa na madhara sawa na dawa za kulevya jamii ya afyuni ambazo ni heroin na morphine, kwani huathiri mfumo wa fahamu pamoja na kusababisha uraibu na vifo vya ghafla.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya dawa hizo pamoja na madhara yanayosababishwa na sumu zilizomo ndani yake, nchi nyingi duniani zimezuia uzalishaji, usafirishaji na matumizi yake.

“Kwa hiyo tunapoona zimeanza kuingia nchini, ni lazima tuongeze juhudi kwenye udhibiti. Wafanyabiashara wanafikiri hizi dawa mpya ni vigumu kuzitambua na hakuna sheria ya kuzishughulikia, sio kweli,” amesema.

Amesema mamlaka hiyo imewezeshwa kupata mtambo unaoweza kupima dawa za kulevya zaidi ya aina 12,000 na hadi sasa dawa mpya zilizopo duniani ni aina 1,300.

“Tunaendelea na kasi ya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo kuendelea kuvunja mitandao ya dawa za kulevya na kubaini mbinu mpya za biashara na matumizi ya dawa hizi,” amesisitiza Kamishna Jenerali Lyimo.

Ripoti ya Hali ya Dawa za Kulevya Duniani 2024 inazitaja dawa mpya za kulevya kuwa hatari zaidi kwa kile kinachoelezwa uzalishaji wake kuiga kemikali zilizopo kwenye dawa za kulevya zinazodhibitiwa kimataifa kama vile bangi, mirungi, heroin na cocaine.

Dawa hizo mpya za kulevya, ikiwemo Mitragyna Speciosa, huzalishwa kwa kuficha uhalisia wake na kukwepa mkono wa sheria.

Ripoti hiyo imebainisha kuwepo kwa matumizi ya mchanganyiko wa dawa za kulevya (cocktail) inayojulikana kwa majina kama “Kush”, “Karkoubi” na “Gutter Water” au “Nyaope”, ambayo mara nyingi huwa na viambata mbalimbali vya dawa za kulevya na dawa tiba zenye asili ya kulevya.

Dawa za heroin, bangi, ketamine, MDMA, methamphetamine, cocaine, caffeine, codeine, morphine, valium, pombe, na viyeyushi zimetajwa kutumika kutengeneza michanganyiko hiyo.

Mchanganyiko huo unaweza kusababisha ulevi uliokithiri, uraibu wa haraka, madhara makubwa ya kiafya na, katika baadhi ya matukio, vifo kutokana na kuzidisha kiasi.