NYOTA 24 wa kikosi cha Yanga wamepaa leo kuifuata Rayon Sports ya Rwanda kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Rayon Sports, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Romain Folz akiitaja safu ya ushambuliaji.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimeiambia Mwanaspoti kuwa kikosi cha Yanga mara baada ya kutua nchini Rwanda kitafikia Park in Hotel mjini Kigali.
“Kikosi cha nyota 24 kinaondoka Dar es Salaam saa kumi jioni na wachezaji wote wapo tayari kwa mchezo kazi ni kwa benchi la ufundi kuhakikisha linamtumia nani na kumuacha nani japo ni muhimu kila mmoja kupata nafasi ya kucheza,” kimesema chanzo kutoka ndani ya timu hiyo.
Kocha Mkuu wa Yanga, Roman Folz amesema kwa wiki chache walizokaa pamoja wachezaji wanaendelea kuzoeana hasa nyota wapya na anapambana kufanya mabadiliko eneo la ushambuliaji ili kutengeneza safu bora.
“Nafurahishwa na juhudi za wachezaji wangu na nimekuwa nikifanya mabadiliko ya mara kwa mara kwenye safu ya ushambuliaji ili niweze kupata mchanganyoko tofauti unaoweza kuzaa mabao mengi,” amesema na kuongeza:
“Kwa ujumla naweza kusema tupo tayari kufanya kwa vitendo kwa kucheza mchezo wa kirafiki wa ushindani na naona nafasi ya kufanya vizuri.”
Akizungumzia mchezo wao na Rayon Sports, amesema wamefanya maandalizi mazuri kwa ajili ya mashabiki, hivyo wanaamini watawapa kitu kizuri na wanaamini wao ndio rasilimali muhimu kwa timu wanatakiwa kufurahia.
“Kwa kuwa wao ni muhimu matarajio ni kuwapa furaha sio tu kwenye mechi dhidi ya Rayon Sports ni kwa ajili ya msimu mzima na naamini watatuunga mkono kwa upendo mkubwa na sisi tunawaahidi furaha kwa kuwapa matokeo mazuri,” amesema.
“Mchezo wetu Ijumaa ni kwa ajili ya kutuweka tayari kwa kuwaandaa wachezaji kimwili na kimbinu baada ya mazoezi ya muda naamini utakuwa kipimo sahihi kwetu na kila mchezaji atapata nafasi ya kucheza.”