Arusha. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru imetoa ufafanuzi wa madai ya mwili wa kijana aliyefariki kutokana na ajali ya pikipiki kuzuiliwa kwa kushindwa kulipa gharama za matibabu ya Sh910,000.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Kipapi Milambo amesema madai hayo hayana ukweli na kwamba mwili haukuzuiliwa, bali kulikuwa na taharuki baada ya baadhi ya marafiki na ndugu wa marehemu kupinga bili waliyopewa.
Tukio hilo lilitokea Agosti 11, 2025, ambapo baadhi ya madereva wa bodaboda na wananchi walikusanyika nje ya chumba cha kuhifadhia maiti wakipinga gharama walizoelezwa kuwa ni matibabu ya marehemu Mohamed Ally (20).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Dk Kipapi, Agosti 9, 2025 saa 4:15 usiku hospitali hiyo ilimpokea Mohamed aliyekuwa amepata ajali ya pikipiki na ndugu zake walifika hospitalini hapo saa 8:00 usiku baada ya kupigiwa simu na wahudumu wa hospitali hiyo.
Amesema, Mohamed kabla hajafariki alifanyiwa uchunguzi ikiwemo kupigwa X-ray, CT Scan na vipimo mbalimbali vya maabara na kutokana na hali aliyokuwa nayo alianzishiwa matibabu ya dharura na kuwekwa chini ya uangalizi maalumu wa daktari.
“Gharama za huduma zote zilizotolewa ilikuwa Sh910,000, ndugu wa mgonjwa walifika ila hali ya mgonjwa ilizidi kubadilika na kwa bahati mbaya pamoja na juhudi zote za kimatibabu zilizofanywa ndani ya kitengo cha huduma za dharura, alifariki dunia,” amesema.
Amesema Agosti 11, 2025 saa 2 asubuhi ndugu wa marehemu walifika kuchukua mwili huo wakiongozana na marafiki wa marehemu (bodaboda), ambapo walipewa bili ya gharama za matibabu na kuelezwa utaratibu wa kulipia wakati mwili ukiandaliwa.
“Wakati wa kuchukua mwili vijana wa bodaboda walifanya vurugu eneo la mochwari wakidai bili waliyopewa ni kubwa na isiyoeleweka. Hospitali inatekeleza maelekezo ya Serikali ya kutozuia miili ya marehemu kwa sababu ya kutolipwa kwa bili, inakanusha taarifa za upotoshaji zenye kuleta taharuki kwamba mwili ulizuiliwa kuchukuliwa,” amesema.
Awali mmoja wa ndugu wa marehemu, Shedy Rajabu alisema walikwenda kuchukua mwili wa ndugu yao kwa ajili ya kwenda kuzika ila walishangaa kukuta gharama kubwa wakati waliambiwa amepelekwa hospitalini akiwa amefariki dunia.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilkiroa, Kata ya Lemara jijini Arusha, alipokuwa akiishi Mohamed, Albert Kilwembwi amesema chanzo cha fujo hizo ni kutokana na gharama hizo kubwa ambapo zilikuwa nje ya uwezo wao.
“Shida kubwa hatukuwa na fedha, tulikuwa tunatafuta namna ya kulipa bili hii, tumeshirikiana na aliyekuwa mwajiri wake na fedha nyingine tumekopa. Wametuchanganulia ila hatuna utaalamu hatuelewi tukaona tutafute namna ya kulipa bili ila hatujaridhika ndiyo maana unaona vijana wameleta taharuki,” amesema Mwenyekiti huyo.