Mkulima wa pamba azawadiwa trekta

Morogoro. Mkazi wa kijiji cha Iputi, kata ya Mbuga wilayani Ulanga, Alifa Bushiri (57) ameibuka kuwa mkulima bora wa zao la pamba kwa kanda ya mashariki baada ya kuvuna kilo 2,723 kwa hekari moja msimu wa mwaka 2024/2025.

Hatua hiyo imemuwezesha kujinyakulia zawadi ya trekta jipya lenye thamani ya Sh53 milioni kutoka Bodi ya Pamba Tanzania (TCB).

Zawadi hiyo ni sehemu ya mpango wa TCB wa kuhamasisha wakulima kuongeza tija kupitia matumizi ya mbinu bora za kilimo, kufuata kanuni za kitaalamu na kutumia mbegu zilizofanyiwa utafiti.

Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 13,2025 Bushiri amesema hakutarajia ushindi huo hadi alipofahamishwa kupitia barua ya mwaliko kuhudhuria maonyesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi kitaifa yaliyofanyika mkoani Dodoma, ambapo alitangazwa mshindi.

“Trekta hili litapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za maandalizi ya mashamba kwa msimu ujao. Nimekuwa nikilima pamba, mahindi na mpunga, lakini kila mwaka nililazimika kukodi trekta kwa gharama ya Sh60,000 kwa hekari. Sasa sitatumia tena Sh720,000 kwa kilimo cha hekari tano za mazao haya.” amesema Bushiri.

Ameeleza kuwa katika hekari tano, alifanikiwa kuvuna kilo 13,615 za pamba, akitumia mfumo wa upandaji wa miche 60-30 uliopendekezwa na watafiti wa zao hilo, huku akizingatia ratiba sahihi za kudhibiti wadudu waharibifu, ikiwemo chawajani.

Ofisa kilimo Mwandamizi wa TCB, Alfonce Ngawagala amesema mkulima anapaswa kuzingatia kanuni 10 za kilimo bora cha pamba, ikiwemo maandalizi ya shamba mapema, matumizi ya mbolea ya samadi, upandaji wa mistari kwa nafasi sahihi, kupunguza miche, kupalilia kwa wakati na kunyunyuzia viuadudu.

“Kufuata kanuni hizi kunaweza kumpatia mkulima mavuno ya zaidi ya kilo 1,500 kwa hekari moja,” amesema Ngawagala.

Kwa upande wake, mtafiti wa pamba kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Methusela Obedy amewataja maadui saba wakuu wa zao la pamba kuwa ni funza mwekundu, funza wa pamba, vidukari, nzi weupe, trips, vidukaziri wadogo na panya shamba akisisitiza umuhimu wa udhibiti wa mapema.