Simulizi ya kukatwa mkono ilivyofufua ndoto ya Matonange

Mwanza. Usilolijua ni kama usiku wa giza. Ndivyo anavyoweza kusimulia tukio la kusikitisha kwa Mwigulu Matonange (21), kijana mwenye ualbino ambaye mwaka 2013 alinusurika kifo baada ya kukatwa mkono na watu wasiojulikana kwa imani za kishirikina.

Wakati huo akiwa na umri wa miaka tisa, akisoma darasa la pili katika Kijiji cha Msia, Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, Mwigulu anasema alikuwa mtoto pekee mwenye ualbino katika kijiji hicho hali iliyomfanya atengwe kijamii, na kukosa ujasiri wa kutembea peke yake.

Mwigulu anasimulia tukio hilo lililotokea baada ya kutoka shule akiwa na binamu yake. Wakiwa njiani, walikutana na wanaume wawili waliovaa nguo nyekundu na nyeupe, wakiwa na mabegi. Ingawa walionekana wa kawaida, macho yao yalionyesha nia nyingine.

“Walisimama darajani wakitutazama kwa muda mrefu, lakini hatukujali kwa kuwa tulikuwa watoto. Tulifika nyumbani, kisha kama kawaida, tukapeleka ndama malishoni. Ndipo tukakutana nao tena,” anasema.

Anaeleza hao watu waliwafuata huku wakiwauliza “Mmetuonea ng’ombe wetu mwekundu?” walipowajibu kuwa hawajamuona, walimwambia Mwigulu awasaidie kuwatafutia, alikataa akisema haoni vizuri kwa sababu ana uoni hafifu, walimlazimisha.

“Mmoja akanibeba mabegani, binamu yangu alipigwa kwa jiwe akakimbia kwenda kutoa taarifa nyumbani,” anasimulia.

Wakiwa wamembeba, Mwigulu alianza kupiga kelele, walimfunika uso kwa nguo, wakamtundika juu ya jiwe akapoteza fahamu, ndipo walipomkata mkono wa kushoto na kuondoka nao.

“Wakati wananikata mkono sikusikia maumivu, huku wakisema “Tufanye haraka kabla watu hawajaja… nafikiri walinipulizia dawa au walinichoma sindano. Walipoondoka na mkono wangu kwenye mabegi yao, ndipo nilipoanza kusikia maumivu,” anasimulia.

Kuokolewa kutoka majeruhi hadi tabasamu

Ndugu yake aliyekimbia kutoa taarifa aliisaidia familia yake kuanza msako wa haraka wanakijiji na ndugu zake waligawanyika maeneo mbalimbali ya msitu huku wakimuita kwa sauti.

“Nikiwa juu ya kilima cha mawe, nilisikia sauti ya kaka yangu akiniita. Nilipoitika, aliniona na kunikuta nikiwa na hali mbaya. Alilia sana akanichukua,” anasimulia.

Baada ya kuokolewa, alipelekwa kituo cha afya kwa huduma ya kwanza, kisha Shirika la Under The Same Sun (UTSS) likampatia msaada wa matibabu, elimu na ushauri wa kisaikolojia. Huku shirika jingine lilimsafirisha nje ya nchi, na kisha kupatiwa mkono wa bandia.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya uzinduzi wa mnara wa heshima kwa watu wenye ualbino katika Kijiji cha Ibisabageni, Wilaya ya Sengerema, Mwanza, amesema tukio lile lilikuwa chachu ya mabadiliko makubwa katika maisha yake.

“Nilipokuwa nasoma zamani sikuwa na ndoto yoyote, nilikwenda shule kukamilisha ratiba tu. Lakini baada ya tukio lile na kupitia changamoto, nilianza kuelewa kuwa maisha yangu yana maana. Nilipewa mkono bandia na kusaidiwa mpaka leo huwa natumia,” anasema.

Kwa sasa, Mwigulu ni mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Baobab, jijini Dar es Salaam anasema ana ndoto ya kuwa mfanyabiashara mkubwa wa kimataifa kutokana na sapoti ya mashirika na watu mbalimbali anayopata.

Licha ya kuwa amepona na kufanikisha baadhi ya malengo yake, Mwigulu bado ana wasiwasi kuhusu usalama wa watu wenye ualbino nchini,

“Ingawa Serikali inajitahidi, bado sijaridhishwa kwa sababu elimu ya kutosha bado haijatolewa. Kuna watoto wenye ualbino wanaogopa kwenda likizo kwa hofu ya kukumbana na vitendo vya ukatili,” anasema kwa msisitizo.

Anaiomba Serikali kuendelea kuimarisha sheria, kutoa elimu vijijini na kuwalinda watoto wenye ualbino kwa karibu zaidi.

“Nawaomba wenzangu wenye ualbino wajikubali, wajitokeze waelimishe jamii. Wasijifiche kwa sababu ya hofu tuna haki ya kuishi kama wengine,” anasema Mwigulu.