KAMATI ya Nidhamu la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imekutana kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nidhamu katika michuano ya CHAN inayoendelea na kutoa uamuzi kadhaa dhidi ya vyama vya soka vya Zambia, Kenya na Morocco.
Katika kikao hicho Shirikisho la Soka Zambia (FAZ) lilipatikana na hatia ya kukiuka Kanuni za vyombo vya habari wakati wa mkutano wa waandishi wa habari kabla ya mechi ya kundi dhidi ya DR Congo.
Zambia ilishindwa kuwakilishwa na kocha mkuu katika mkutano huo wa lazima wa kabla ya mechi. Kwa kosa hilo imetozwa faini ya Dola 5,000 (takriban Sh12.7 milioni).
Kwa upande mwingine, Shirikisho la Soka Kenya (FKF) limepatikana na makosa kadhaa ya kiusalama wakati wa mechi dhidi ya Morocco iliyofanyika katika Uwanja wa Moi – Kasarani.
CAF ilisema Kenya ilishindwa kutimiza masharti ya usalama na hivyo kutozwa faini ya Dola 50,000 (takriban Sh127 milioni).
Pia CAF imeonya kuwa endapo hali hiyo itaendelea mechi za timu ya taifa ya Kenya zinaweza kuhamishiwa katika uwanja mbadala.
Pia Kenya imetakiwa kuongeza idadi ya askari kwenye eneo la uwanja na kuhakikisha barabara zinazouzunguka zinafungwa ipasavyo siku za mechi. Vilevile, Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) limeadhibiwa kutokana na tabia isiyofaa ya wachezaji katika mechi hiyo dhidi ya Kenya.
Morocco imetozwa faini ya Dola 5,000, ambapo Dola 2,500 kati ya hizo imesamehewa kwa masharti kwamba kosa kama hilo halitarudiwa.