MCHEZAJI wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, Dimeji Lawal, ameonyesha kutoridhishwa kwake na kiwango cha Nigeria (Home-Based Eagles) baada ya kutolewa kwenye michuano ya CHAN huku akiipongeza Taifa Stars ya Tanzania.
Nigeria ilikumbana na kipigo kizito cha mabao 4-0 kutoka kwa Sudan katika mechi yao ua pili ya kundi D, iliyopigwa Jumanne. Kabla ya kipigo hicho, ilikuwa imefungwa bao 1-0 na Senegal katika mechi ya kwanza.
Akizungumza na Mwanaspoti mara baada ya kipigo cha kusikitisha kutoka kwa Sudan, Lawal alionyesha kushangazwa na kiwango cha wachezaji wa ndani katika mechi hiyo.
“Nimevunjika moyo sana kuona Nigeria ikishindwa kuvuka hatua ya makundi kwenye CHAN inayoendelea,” alisema Lawal.
“Hii ilikuwa nafasi ya wachezaji kujidhihirisha kwa kocha mkuu wa Super Eagles, Eric Chelle, kwamba wanastahili kupewa nafasi kwenye kikosi cha kwanza. Lakini kwa kiwango hiki, hasa dhidi ya timu ya Sudan, sina uhakika kama wamejiwekea sifa yoyote.”
Akiendelea, Lawal alisema: “Ninaipongeza Tanzania kwa namna Taifa Stars ilivyojituma na kuonyesha mshikamano wa kweli wa timu. Hii inaonyesha mpira wa Afrika Mashariki unakua kwa kasi.”
Lawal aliongeza kuwa matokeo hayo kwa Nigeria yanadhihirisha upungufu katika maandalizi na ari ya kupambana kwa wachezaji.
Alisema baadhi ya wachezaji walionekana kukata tamaa mapema, jambo lililoipa Sudan nafasi ya kutawala mechi.
Kwa mujibu wake mechi ya mwisho ya kundi dhidi ya Congo sasa itabaki kuwa ya heshima tu, kwani Nigeria haina nafasi ya kuendelea mbele. “Hawana cha kupoteza sasa, wanapaswa kupambana kwa heshima yao binafsi na ya taifa,” alisema.