Arusha. Wakati vyama mbalimbali nchini vikiendelea na michakato yake ya ndani kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilaya ya Arusha Mjini, kimewafuta uanachama wanachama wake 12 wanaotuhumiwa kukisaliti chama hicho.
Miongoni mwa waliokumbana na adhabu hiyo ni Amina Abubakar na Linus Agustino (hamasa/walinzi wa chama), ambao wamedaiwa kwa nyakati tofauti kati ya Mei na Juni 2025 wamekuwa wakitengeneza mtandao ndani ya chama katika Jimbo la Arusha Mjini , kuhakikisha baadhi ya wanachama wanahamia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).
Taarifa kwa umma iliyotolewa Agosti 12, 2025 na Katibu wa Chadema Wilaya ya Arusha Mjini, Francis Chuma, imeeleza kikao chake cha kawaida cha kamati tendaji ya wilaya kilichofanyika Agosti 2, 2025 chini ya Mwenyekiti, Ricky Moiro, pamoja na mambo mengine kilikuwa na mashauri ya kinidhamu ya baadhi ya wanachama na viongozi wake.
Taarifa hiyo imeeleza kikao hicho kimejadili na kuazimia kwa pamoja kuwachukulia hatua za kinidhamu baadhi ya viongozi na wanachama kutokana na mwenendo usioendana na katiba, itikadi, falsafa na madhumuni ya Chadema ya mwaka 2006 toleo la 2019.
Amedai kuwa wanachama hao wawili walipatikana na hatia katika makosa ya usaliti juu ya chama na wamekuwa wakitenda makosa hayo wakijua siyo halali kujishughulisha na shughuli za chama kingine.
Amesema wanachama hao wamekutwa na hatia kwa mujibu wa Katiba ya Chadema ibara ya 5.1,5.2.6 na ibara ya 5.3,5.3.3,5.3.4 na Kanuni za maadili ya mwanachama 10.3 (iii) na Kanuni za maadili (a) usaliti (i),(ii) na (.iv).
Taarifa hiyo imeeleza wanachama wengine waliofukuzwa ni Boniphas Kimario aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Sekei, Hamisi Kidoleso na aliyewahi kuwa katibu wa kata hiyo, Emmanuel Assey.
“Hawa wamepatikana na hatia katika makosa mbalimbali waliyokuwa wanajihusisha nayo toka mwaka 2024 yaliyo kinyume na katiba, kanuni, maadili na miongozo ya Chadema ya mwaka 2006 toleo la 2019,”imesema taarifa hiyo.
Wengine waliofukuzwa ni aliyekuwa mhazini wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Emma Kimambo na aliyewahi kuwa katibu wa Bawacha Kata ya Unga Ltd, Martha Masoi, ambao walijiondoa na kujiunga na chama kingine wakati mashauri yao ya kinidhamu yakiendelea.
Taarifa hiyo imewataja wengine ni John Lema, Amani Kimath ambaye aliwahi kuwa Katibu Mwenezi wa Kata ya Sombetini, Shaban Mipilo, Jacklin Kimambo na Selemani Ally ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Kata ya Elerai(amejiunga na CCM) na kuwa hao siyo viongozi wala wanachama wa Chadema kwa sababu walijiunga na vyama vingine.
“Chadema Jimbo la Arusha Mjini kinapenda kukumbusha kuwa tunaelewa kujiunga na vyama vya siasa ni hiari ulimwenguni, hivyo hakitazuia hiari ya mwanachama kutoka, lakini siyo ruhusa wala haikubaliki na haitakubalika wala kuvumilika kuwa na wanachama wa Chadema huku unakifanyia kazi chama kingine,”imeeleza.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa chama hicho hakitasita kuchukua hatua za juu za kujilinda dhidi ya uadilifu wake kwa mujibu wa katiba, kanuni na maadili ya chama.
“Hata hivyo ifahamike kuwa uadilifu, uaminifu, utiifu na uzingatiaji wa maadili ya chama ni msingi imara wa chama chochote makini cha siasa, hata siku moja chama hakitamvumilia mwanachama/wanachama anayetaka kukifanyia biashara kwa masilahi yake binafsi,”imeeleza taarifa hiyo.
“Kama chama tunaamini siasa ni mchakato wa jamii kujiamulia mambo yake kwa masilahi ya jamii nzima kwa kupitia njia za kidemokrasia, na siyo njia ya mkato ya kuhalalisha masilahi ya watu/mtu binafsi au kikundi cha watu binafsi,”
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Emma aliyekuwa Mhazini wa Chadema ameeleza kuwa kabla ya kuhama chama hicho aliandikiwa barua na tawi la Olkeriab, kuhusu tuhuma za usaliti na kuwa kutokana na wadhifa wake shauri lolote dhidi yake linapaswa kusimamiwa na ngazi ya juu (Kamati Kuu).
“Mimi ni miongoni mwa G55,nilikuwa natuhumiwa kuwa nimeenda kinyume na taratibu za chama, niliandikiwa barua na tawi, nikawakosoa nikawaambia kama nina tuhuma waelekeze ngazi yangu ya kinidhamu ambayo ni kamati kuu ili nichukuliwe hatua,lakini hawakufanya hivyo,”
“Jimbo au tawi haliwezi kuwa na mamlaka kuniadhibu, mimi nilishaondoka Chadema tena hadharani tangu Mei 21,2025,na nikasema nisihusishwe na masuala yoyote ya Chadema. Hii taarifa yao ni kama wanatafuta kiki sioni kama kuna haja ya kujibu,”ameeleza Emma