Majaliwa akagua miundombinu mabasi ya mwendokasi Mbagala, atoa maagizo

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametembelea na kukagua miundombinu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) katika Barabara ya Kilwa na kuagiza kazi iliyosalia ikamilishwe ili huduma hiyo ianze kutolewa mwezi huu.

Majaliwa amefanya ziara hiyo leo Jumatano Agosti 13, 2025, zikiwa zimepita siku sita tangu Mwananchi iliporipoti uharibifu na kasoro mbalimbali kwenye miundombinu hiyo, ilikamilika miaka miwili iliyopita.

New Content Item (1)

Hali hiyo ilibainika wakati mabasi 99 kati ya 250 yatakayotumika katika awamu ya kwanza kwenye barabara hiyo kati ya mbagala na katikati ya Jiji la Dar es Salaam, yakiwa yamewasili nchini.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, sehemu mojawapo ambayo ilibainika ina kasoro ni kutokamilika kipande cha Kamata, Kariakoo.

Hata hivyo alipoulizwa Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Athuman Kihamia alisema mabasi hayo yakianza kazi yatatumia barabara za kawaida yanapopita magari mengine kwa sasa hadi hapo njia zake zitakapokamilika.

Mbali na eneo hilo, pia katika vituo hakuna miundombinu ya mageti janja inayoruhusu abiria kukata tiketi wala kuzikagua kidijitali kwa kutumia kadi.

Vilevile baadhi ya miundombinu ilibainika imeanza kuharibika, zikiwemo taa za kuongozea magari huku nyingine zikiwa zimepasuka kwa kile kilichoelezwa ni kutokana na magari yenye urefu mkubwa kupita maeneo hayo, mengi yakiwa ni kutokea bandarini.
 

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Alichosema Waziri Mkuu
Akiwa katika ziara yake leo, Waziri Majaliwa amewataka amewaagiza waendeshaji wa awamu ya pili ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT-2) kuhakikisha wanafanyakazi usiku na mchana ili kukamilisha maeneo yaliyobaki yatakayowezesha mradi huo kuanza kutoa huduma ndani ya muda mfupi.

“Tunataka mradi huu uanze kutoa huduma kwa Watanzania hasa wakazi wa Dar es salaam, mradi huu utaongeza ufanisi wa usafiri wa umma katika jijini la Dar es Salaam na kutoa huduma ya kisasa, salama na ya haraka kwa wananchi,” amesema.

Kadhalika, Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya utoaji huduma ya Usafiri ya Mofat, Mohammad Kassim kuhakikisha anakamilisha haraka taratibu za utoaji wa mabasi 99 yaliyopo bandarini ili kuwezesha huduma hiyo kuanza kwa wakati.

Majaliwa amesema Serikali  inataka kuona katika awamu ya pili ya mradi wa BRT, tiketi za usafiri kupitia mabasi hayo zinakuwa za kielektoniki badala ya tiketi za karatasi kama ilivyokuwa awali. “Tukifanya hivi itatusaidia kumonitor kiasi cha fedha kinachokusanywa.”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa za ajira zitakazotokana na mradi huo ikiwemo udereva. 

“Nendeni mkasome masuala ya udereva kupitia Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), mradi huu utahitaji idadi kubwa ya madereva wenye ujuzi.”
Katika ziara hiyo pia Waziri Mkuu amekagua mabasi hayo, kituo maalumu cha kujazia gesi kwa ajili ya mabasi hayo, kinachojengwa katika eneo la Mbagala Rangi Tatu.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Mabasi yaliyowasili, mali ya Kampuni ya Mofat, ni sehemu ya mabasi 250 yatakayotoa huduma katika njia hiyo, ikiwa ni utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo, ikiwa imepewa mkataba wa miaka 12.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 20.3 kati ya Mbagala hadi Gerezani, ilijengwa na Kampuni ya Sinohydro China na ilikabidhiwa kwa Dart Agosti 2023. 

Katika ziara hiyo Majaliwa ameambatana na na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi; Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, (Tamisemi), Zainab Katimba na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk Jim Yonazi.

Wengine waliokuwepo kwenye msafara huo ni watendaji wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na Chuo cha Taifa cha usafirishaji (NIT).