Dodoma. Shirika lisilo la kiserikali la World Vision Tanzania (WVT) limezindua kampeni ya uhamasishaji jamii ambayo inalenga kuchangia chakula shuleni.
KampeniĀ hiyo imebuniwa kwa ajili ya kushawishi mahudhurio ya wanafunzi, kupunguza utoro na utapiamlo kwa watoto.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Agosti 13, 2025 Mkurugenzi wa World Vision Tanzania, James Anditi amesema kupitia kampeni hiyo kuongeza lishe ya watoto na kuboresha mahudhurio ya wanafunzi shuleni ikiwemo utendaji.
Anditi amesema licha ya faida zilizothibitishwa katika milo ya shule, kuna uboreshaji mahudhurio, utendaji wa masomo na lishe ya watoto.
“Changamoto hii inaongezewa na ufahamu mdogo kati ya wazazi, viongozi wa imani, na watunga sera juu ya thamani ya muda mrefu ya kuwekeza katika mipango ya kulisha shule,” amesema Anditi.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa, kampeni hiyo inaongozwa na wizara muhimu za Serikali na washirika wa maendeleo kwa ushirikiano wa mashirika ya jamii, shule, viongozi wa imani na vyombo vya habari.
Amesema wakati wote mwanafunzi mwenye njaa huwa hafundishiki ukilinganisha na wanaopata chakula walau cha mchana.
Mwalimu Gaudensia Chomola amesema shughuli zinazofanywa kwenye mpango huo zitalingana na miongozo ya kulisha shule za kitaifa, sera ya kitaifa ya chakula na lishe, na mpango wa maendeleo ya sekta ya elimu 2025/26 hadi 2029/30.
Chomola amesema mpango wa kulisha shule nchini Tanzania, utakuwa muhimu katika kuboresha mahudhurio ya wanafunzi na namna bora ya ujifunzaji kwa wanafunzi.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi, Samson Samwel amesema mkakati huo unapaswa kushirikishwa zaidi kwa wazazi kwani wakitambua umuhimu wa chakula itawasaidia.