Shinyanga. Ikiwa ni siku ya tatu tangu watu 25 wafukiwe chini ya ardhi katika mgodi wa wachimbaji wa dhahabu wa kikundi cha Wachapakazi wa Gold Mine, ulioko katika Kijiji cha Mwongozo, mkoani Shinyanga, baadhi ya ndugu wa waathirika wameiomba Serikali kuongeza juhudi za uokoaji ili kuwaokoa wapendwa wao wakiwa hai.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amesema amepokea ombi hilo na kuweka kambi ya madaktari ambao watatoa huduma ya kwanza kwa haraka kabla ya kupelekwa hospitali.
“Ombi lenu nimelipokea na kuanzia sasa baadhi ya madaktari wataweka kambi hapa ili kutoa huduma ya kwanza kwa haraka zaidi kabla ya ndugu zetu kufikishwa hospitalini,” amesema Mhita.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Agosti 13, 2025, katika eneo la tukio, baadhi ya ndugu wa watu waliokwama mgodini wamepongeza juhudi za waokoaji, wakisema kuwa wanajitahidi kufanya kazi usiku na mchana kwa zamu bila kupumzika.
Mkazi wa Kisesa, mkoani Mwanza, Catherine Koregeja, ambaye ni mmoja wa waliowasili kwa ajili ya kufuatilia hatima ya ndugu yake, amesema kuwa hadi sasa mjomba wake bado yuko chini ya ardhi.
“Mara ya mwisho kuwasiliana na mjomba ni Jumamosi tulizungumza kuhusu kuja harusini lakini hakuja na baadaye simu yake ikawa haipatikani, Jumatatu ndio tukapata taarifa kuna maduara yametitia katika mgodi anaofanya kazi,” amesema Catherine mmoja wa waliofika kusubiri hatima ya jamaa zao waliofukiwa na mgodi huo.
“Waliopo chini ni vijana wangu wawili ambao walikua wanafanya kazi hapa, toka tumesikia hii ajali tumefika hapa juhudi za uokoaji zinaridhisha, lakini tunaiomba Serikali iongeze juhudi na wataalamu zaidi na madaktari ili basi ndugu zetu waweze kutoka wakiwa hai,” amesema Joseph Buzuga.

Watu hao 25 wamefukiwa chini ya ardhi baada ya maduara matatu ya uchimbaji dhahabu yaliyokuwa yakifanyiwa ukarabati kutitia katika mgodi wa Wachapakazi wa Gold Mine, uliopo Kijiji cha Mwongozo, Kata ya Mwenge, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Chifu Inspekta wa kikundi kinachomiliki mgodi huo, Fikiri Mnwagi, maduara hayo matatu yalikuwa katika hatua ya ukarabati wakati ardhi ilipotitia ghafla na kuwafunika watu 25, wakiwemo wafanyakazi na mafundi.
Kwa mujibu wa Mnwagi ajali hiyo imetokea Agosti 11, 2025, saa nne asubuhi ambapo kati ya watu waliofukiwa, wanne walikuwa ndani ya duara namba 20, wengine 11 walikuwa katika duara namba 103, na sita walikuwa katika duara namba 106.
Juzi Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro alifika kwenye eneo la tukio na aliwaomba wananchi wawe watulivu wakati uokoaji ukiendelea.