Sh769.4 zilivyomaliza kero ya maji Sapiwi, Mwandama

Bariadi. Zaidi ya wakazi 6,865 wa vijiji vya Sapiwi na Mwandama katika halmashauri ya wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu,wameondokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama baada ya mradi wa maji wa Sapiwi kukamilika.

Mradi huo ambao umezinduliwa leo, Agosti 13,2025 wakati wa mbio za mwenge wa uhuru wilayani  hapa, umegharimu Sh769.4 milioni hadi kukamilika kwake, umetajwa kuondoa adha kubwa ya maji ambayo wananchi walikuwa wakikabiliana nayo.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (Ruwasa) wilayani Bariadi, Moses Mwampunga amesema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa Machi 26,2023 na kukamilika Machi 11,2024 .

Aidha amesema wilaya hiyo imekuwa ikichukua hatua za makusudi ili kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi, ambapo kutokana na jitihada hizo upatikanaji wa huduma hiyo umeongezeka kutoka asilimia 64 hadi asilimia 80.9.

“Mradi huu wa maji wa Sapiwi unatoa huduma kwa wananchi 6,865 wa vijiji vya Sapiwi na Mwandama na una uwezo wa kuzalisha maji lita 197,000 kwa siku, lakini wilaya hii inaendelea kufanya jitihada ili kuongeza mtandao wa maji ndani ya wilaya kwa kutekeleza miradi ya mbalimbali ya maji,”

“Mradi umekamilika pia ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa kubeba lita 90,000 kwenye mnara wa mita 12,vituo 16 vya kuchotea maji na birika moja la kunyweshea maji mifugo vimejengwa,”amesema.

Akizungumza kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2025,Ismail Ussi  amesema kuwa mradi huo ni moja ya jitihada za Serikali kuhakikisha inawafikishia huduma ya maji safi na salama wananchi katika maeneo ya vijiji.

“Baada ya kupokea taarifa ya kina inayohusiana na mradi huu wa maji na kufanya ukaguzi tumeona kazi nzuri imefanyika, tunawapongeza viongozi kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya pamoja na ndugu zetu wa Ruwasa,”amesema.

Mariam Nyamogo, mkazi wa Kijiji cha Sapiwi amesema kabla ya mradi huo walilazimika kutembea zaidi ya kilomita tano kutafuta maji kwenye visima vya asili ambavyo mara nyingi maji yake hayakuwa salama.

“Tulikuwa tunapoteza muda mwingi kutafuta maji, hasa wanawake na watoto. Sasa tunapata maji karibu na nyumbani, tutapata muda wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo,” amesema.

Naye Daudi Masalu, mkazi wa Kijiji cha Mwandama, amesema afya zetu zitakuwa bora kwa sababu sasa tunapata maji safi kutoka kwenye bomba. Tunashukuru sana Serikali na wadau wote,” amesema.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi ambapo mwenge umepokelewa ukitokea halmashauri ya mji wa Bariadi, umekimbizwa kilomita 184 ambapo umetembelea, kukagua na kuzindua  miradi sita yenye thamani ya Sh1.5 bilioni.