Mwanza. Kamisheni ya Ziwa Victoria (LVBC), imesema ujenzi wa meli mpya ya MV New Mwanza ‘Hapa Kazi Tu’ na maboresho ya miundombinu ya bandari jijini Mwanza ni hatua itakayobadilisha sura ya usafirishaji na biashara katika Ziwa Victoria, huku ikifungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kimaeneo.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano, Agosti 13, 2025, jijini Mwanza na Katibu Mtendaji wa LVBC, Dk Masinde Bwire wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Uganda, Edith Mwaje, ambaye alikuja kujionea maendeleo ya miradi ya usafiri wa majini na reli katika jiji hilo.
Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Uganda, Edith Mwaje akishuka ndani ya New Mv Mwanza Hapa Kazi Tu baada ya kuitembelea na kuikagua ndani.
Ziara hiyo ya siku tatu, imehusisha kutembelea bandari ya Mwanza Kusini na Kaskazini, pamoja na kushuhudia vyombo vya kisasa vilivyonunuliwa na jumuiya hiyo kwa ajili ya kuboresha huduma za majini, ikiwemo boti ya kubebea wagonjwa na boti ya utafiti.
Dk Bwire amesema Kamisheni ya Ziwa Victoria inatekeleza mpango wa kimkakati wa kuunganisha miundombinu ya usafiri kwenye ziwa hilo kwa njia ya maji, reli na barabara, ili kurahisisha safari za abiria na usafirishaji wa mizigo.

Katibu Mtendaji wa LVBC, Dk Masinde Bwire (watatu kushoto) akizungumza jambo wakati wa ziara ya kuitembelea na kukagua boti ya utafiti ya Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria katika bandari ya Mwanza Kusini jijini Mwanza. Picha na Saada Amir.
Amesema juhudi hizo zinalenga si tu kuinua biashara, bali pia kuongeza mshikamano wa kijamii na kukuza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Tanzania, Uganda na Kenya.
“Leo tumetembelea bandari ya Mwanza Kaskazini na kuona miundombinu ya kisasa inayojengwa. Tunashukuru Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huu mkubwa.
“MV Mwanza ni meli ya kipekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki.. hakuna meli bora zaidi ya hii hapa, ukiondoa zile kutoka Ulaya. Tunataka juhudi hizi ziunganishwe na uwekezaji wa Uganda na Kenya ili wananchi waendelee kunufaika na usafiri salama, biashara yenye tija na safari bora,” amesema Dk Bwire.

Katibu Mtendaji wa LVBC, Dk Masinde Bwire (kulia) akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Uganda, Edith Mwaje (kushoto) wakati wakipewa maelezo ya ujenzi wa Meli ya New Mv Mwanza ‘Hapa Kazi Tu’
Ameeleza kuwa meli hiyo haitabeba tu abiria na mizigo, bali pia itakuwa kichocheo cha utalii, kwa kuwa itarahisisha safari kati ya miji mikubwa kando ya Ziwa Victoria, ikiwemo Mwanza, Bukoba, Kampala na Kisumu.
Kwa upande wake, Edith Mwaje ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa ujenzi wa meli hiyo, akisema atapeleka taarifa kwa Serikali ya Uganda kuhusu hatua kubwa zilizopigwa, ili nchi hizo mbili ziendelee kushirikiana katika kuboresha miundombinu na kuongeza kiwango cha biashara ya mipakani.
“Mv Mwanza nadhani itarahisisha usafiri kati ya Kampala na Mwanza. Nitarudi na ripoti hii kwa Serikali ya Uganda ili kuwaambia kwamba mengi yanafanywa hapa, yote yanalenga kufanya biashara pamoja kati ya Tanzania na Uganda.
“Tutazingatia hatua zilizofikiwa katika kurahisisha uunganishaji, kuongeza biashara na usafirishaji kwenye Ziwa Victoria,” amesema Mwaje.
MV New Mwanza iliyoanza kujengwa mwaka 2020 na mkandarasi wa Kampuni ya Gas Entec Ship-Building Engineering ya Korea kwa gharama ya zaidi ya Sh124 bilioni, imefikia asilimia 98.
Meli hiyo inayotajwa kuwa kubwa zaidi kuliko zote katika Ziwa Victoria, itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari 20 na malori matatu, ikiwa na ghorofa nne, uzito wa tani 3, 500, urefu wa mita 92.6 na upana wa mita 17.
Itafanya safari zake kati ya Bandari za Mwanza, Kemondo, Bukoba, Portbail nchini Uganda na Kisumu nchini Kenya.
Meli ya MV New Mwanza ‘Hapa Kazi Tu’ itakuwa na madaraja tofauti kwa ajili ya abiria kulingana na mahitaji na uwezo wao kiuchumi.

Baadhi ya viongozi wakitoka kukagua boti ya kubebea wagonjwa katika bandari ya Mwanza Kaskazini jijini Mwanza. Picha na Saada Amir
Ndani ya meli hiyo, kutakuwa na daraja la hadhi ya juu (VVIP) lenye uwezo wa kuhudumia abiria wawili, daraja la watu mashuhuri (VIP) litakalobeba abiria wanne, daraja la kwanza litakalohudumia abiria 60 na daraja la biashara litakalobeba abiria 100.
Madaraja mengine ni la pili litakalotumiwa na abiria 200 na daraja la uchumi litakalobeba abiria 836.
Lifti yenye uwezo wa kubeba watu 20 kwa wakati mmoja ni huduma nyingine maalumu itakayopatikana ndani ya meli hiyo kwa ajili ya abiria wenye changamoto za kiafya na viungo.
Abiria wenye matatizo na dharura za kiafya wawapo safarini watapata huduma ya vipimo na tiba katika zahanati maalumu iliyomo ndani ya meli huku, wajawazito na wanaonyonyesha nao wakitengewa eneo maalumu wakati wa safari.
Wanaotaka kufunga ndoa na kufanya sherehe wakiwa safarini ndani ya meli nao watapata fursa kutokana na meli hiyo kuwa na ukumbi maalumu wa sherehe na burudani.