Andrew Chamungu atua Namungo FC

ALIYEKUWA mshambuliaji wa Songea United, Andrew Chamungu amekamilisha usajili wa kujiunga na Namungo, huku nyota huyo akipewa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine.

Chamungu aliyewahi kutamba na timu mbalimbali zikiwamo za, Polisi Tanzania, Mbuni na Kitayosce ambayo kwa sasa ni Tabora United, amekamilisha dili hilo la kujiunga na kikosi hicho na sasa kinachosubiriwa ni utambulisho rasmi kwa nyota huyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chamungu alisema kuna baadhi ya timu ambazo anafanya mazungumzo nazo, ingawa kwa sasa hawezi kuweka wazi ni wapi atacheza msimu ujao, japo mashabiki wake wamtarajie akicheza Ligi Kuu Bara na sio Championship tena.

“Nafikiri ni muda wa kutafuta changamoto sehemu nyingine, nimecheza pia Championship vya kutosha na sasa naona ni wakati sahihi wa Ligi Kuu Bara, siwezi kusema ni klabu gani nitacheza ila mambo yakikamilika yatakuwa wazi,” alisema Chamungu.

Licha ya kauli hiyo ya nyota huyo aliyetamba pia na Lipuli FC na FGA Talents FC ambayo kwa sasa ni Fountain Gate FC, Mwanaspoti linatambua Chamungu ameshajiunga na Namungo kwa lengo la kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji la kikosi hicho.

Msimu wa 2024-2025, katika Ligi ya Championship mshambuliaji huyo aliifungia Songea United mabao tisa, huku akikiwezesha kikosi hicho kumaliza katika nafasi ya sita na pointi zake 52, baada ya kushinda mechi 15, sare saba na kupoteza nane.

Chamungu anaungana na nyota mwenzake, Cyprian Kipenye aliyetokea pia Songea United na mshambuliaji mwingine, Abdulaziz Shahame ‘Haaland’, kutoka TMA FC ambapo wote walicheza Championship kwa msimu wa 2024-2025 na kuonyesha viwango vizuri.