REKODI ni rekodi tu, haijalishi nzuri au mbaya. Unaweza kusema hivyo kufuatia kilichotokea kwa timu ya Taifa ya Tanzania maarufu Taifa Stars na ile ya Nigeria ijulikanayo kwa jina la Super Eagles.
Timu hizo mbili hadi kufikia usiku wa Agosti 12, 2025 ndiyo pekee zilikuwa zinafahamu zimevuna nini kwenye michuano ya Chan 2024 inayoendelea kuchezwa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, huku zilizobaki zikisubiri hatma zao mechi zijazo.
Tanzania iliyopo Kundi B ikicheza mechi zake Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, imeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kufuzu robo fainali ya michuano hiyo kufuatia kushinda mechi tatu mfululizo na kukusanya pointi tisa ikiwa kileleni.
Pointi hizo zinaifanya Tanzania kujihakikisha kucheza robo fainali kwa kumaliza kinara wa kundi licha ya kubakiza mechi moja dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati itakayopigwa Agosti 16 mwaka huu.
Uhakika wa Tanzania kumaliza kinara wa Kundi B unatokana na pointi tisa ilizonazo zinaweza kufikiwa na Burkina Faso pekee endapo ikishinda mechi zake mbili kutokana na sasa kukusanya pointi tatu, lakini kanuni ya matokeo timu hizo zilipokutana zinaibeba Stars kwani iliichapa Burkina Faso 2-0 mechi ya ufunguzi.
Kwa upande wa Nigeria iliyopo Kundi D huku mechi zake ikicheza Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar, imeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kuondoshwa mashindanoni.
Licha ya kwamba bado ina mechi moja ya kucheza dhidi ya Congo itakayofanyika Agosti 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar, lakini Nigeria haiwezi kufuzu robo fainali kutokana na nafasi iliyopo. Nigeria inaburuza mkia wa Kundi D ikiwa haina pointi baada ya kupoteza mechi mbili ikianza kufungwa 1-0 na Senegal, kisha kichapo cha 4-0 kutoka kwa Sudan.
Baada ya kumalizika hatua ya makundi, timu mbili za juu kwa kila kundi zitafuzu robo fainali. Katika hatua ya robo fainali, kinara wa kundi A atacheza na aliyeshika nafasi ya pili kundi B mechi ikipigwa Uwanja wa Moi Kasarani nchini Kenya, huku kinara wa kundi B akicheza na aliyeshika nafasi ya pili kundi A kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar. Hizi zitafanyika Agosti 22 mwaka huu.
Pia kinara wa kundi C atacheza na aliyeshika nafasi ya pili kundi D mechi ikifanyika Uwanja wa Amaan kisiwani Zanzibar, kisha kinara wa kundi D akicheza na aliyeshika nafasi ya pili kundi C pale Uwanja wa Mandela nchini Uganda. Hizi zitapigwa Agosti 23 mwaka huu.