Msako mwingine robo fainali kupigwa leo

MSAKO wa kuisaka tiketi ya kucheza robo fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), inaendelea leo kwa mechi mbili za kundi A kupigwa ambapo Morocco itacheza na Zambia inayoburuza mkiani.

Mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Kasarani, Nairobi itapigwa kuanzia saa 11:00 jioni kisha mtanange mwingine wa kundi A kati ya Angola dhidi ya DR Congo utaanza saa 2:00 usiku.

Morocco imecheza mechi mbili hadi sasa na kukusanya pointi tatu, ambapo kati ya hizo imeshinda moja tu baada ya kuifunga Angola mabao 2-0, kisha kuchapwa na wenyeji Kenya bao 1-0, huku kwa upande wa Zambia ikisaka ushindi wake wa kwanza leo.

Zambia imechapwa mechi zote mbili ilizocheza hadi sasa baada ya kuchapwa mabao 2-0, dhidi ya DR Congo, kisha ikapoteza tena kwa mabao 2-1, mbele ya Angola, hivyo kuhitaji ushindi pekee leo ili angalau iweze kufufua matumaini ya kundi hilo.

Kwa upande wa Angola inayoshika nafasi ya pili na pointi nne nyuma ya vinara Kenya yenye pointi saba, katika mechi tatu ilizocheza imekuwa na matokeo mchanganyiko baada ya kikosi hicho kushinda moja, kikitoka sare moja na kupoteza pia moja.

Angola ilianza michuano hiyo kwa kichapo cha mabao 2-0, kutoka kwa Morocco, huku mechi ya pili ikatoka sare ya kufungana bao 1-1, dhidi ya wenyeji Kenya, kisha kikafufua matumaini ya ushindi wa kwanza, baada ya kuichapa Zambia kwa mabao 2-1.

Kwa upande wa DR Congo iliyo nafasi ya nne na pointi tatu, imecheza mechi mbili hadi sasa, ambapo ilianza michuano hii kwa kuchapwa na wenyeji Kenya bao 1-0, kisha ikajiuliza vizuri mbele ya vibonde Zambia baada ya kuitandika pia mabao 2-0.

Katika kundi hili la A, Zambia ndio timu pekee ambayo haijashinda mechi yoyote, huku pia ikikumbana na changamoto kubwa ya safu ya ushambuliaji, kwani kikosi hicho hadi sasa kimefunga bao moja tu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne. Kenya iliyo na nafasi kubwa ya kuongoza kundi na kukutana na Tanzania katika hatua ya robo fainali, inaongoza na pointi saba, ikifuatiwa na Angola yenye pointi nne, huku Morocco na DR Congo zilizo nafasi ya tatu na nne zikiwa na pointi tatu.