Skauti West Ham akodolea macho CHAN

MASHINDANO ya CHAN 2024 yanaendelea kuwavuta wadau mbalimbali wa soka wakiwemo maskauti kutoka kila pembe ya dunia kwa ajili ya kutazama vipaji vya ndani katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Miongoni mwa waliokuwa wakifuatilia kwa karibu mechi za Taifa Stars katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ni pamoja na Charton, mchunguzi wa vipaji (scout) kutoka London anayefanya kazi chini ya kocha wa zamani wa Chelsea, Graham Potter ambaye sasa anakinoa kikosi cha West Ham United.

Charton ambaye anadai kuwa chini ya Kyle Macaulay, mkuu wa usajili wa West Ham aliwasili nchini wiki iliyopita akiwa na lengo maalumu la kusaka wachezaji chipukizi wa viwango vya juu wanaoshiriki CHAN 2024.

Tofauti na watu wengi maarufu wanaopenda kuonekana mbele ya kamera, Charton hakutaka kuwa karibu na wanahabari hapa Zanzibar ambako alikuwa akitazama mechi ya kundi D.

Licha ya hayo, miongoni mwa wachezaji waliomvutia skauti huyo ni pamoja na Clement Mzize ambaye alipachika mabao mawili katika mechi iliyopita dhidi ya Madagascar.

Kwa mujibu wa taarifa West Ham inaweza kumualika Mzize kwenye majaribio maalum Ulaya, ikiwa ataendelea kudhihirisha kiwango chake hadi mwisho wa mashindano.

Pia kuna taarifa kwamba klabu za Ubelgiji na Uholanzi zimeonyesha nia ya kushirikiana na West Ham katika programu za kukuza vipaji kutoka Afrika.

Charton anatarajiwa kusalia nchini hadi mwisho wa mwezi huu, akifuatilia mechi zote za Taifa Stars na pia kutembelea vituo vya kukuza vipaji vilivyopo mikoani.