Azam FC yashusha Mtunisia | Mwanaspoti

HUENDA Azam FC ikimtambulisha mshambuliaji, Baraket Hmidi Agosti 15 na anatarajia kuingia nchini muda wowote kwa ajili ya kukamilisha taratibu za vipimo ili aweze kuungana na wenzake waliopo kambini Arusha, kujiandaa na msimu mpya.

Chanzo cha ndani kilisema Azam imemsajili Hmidi kutoka klabu ya CS Sfaxien na ilielezwa huenda akawa wa mwisho na baada ya hapo litafuata zoezi la kuachana na baadhi ya wachezaji ambao hawatakuwa katika mpango wa kocha Florent Ibenge.

Hmidi aliyezaliwa Februari Mosi, 2003 (umri 22) nchini Tunisia ana uwezo wa kucheza nafasi zote za mbele, kutokea kulia, kushoto na kati, jambo ambalo alikuwa analitaka kocha Ibenge na ndiyo sababu ya kumrejesha beki anayecheza kushoto na Kati, Edward Charles Manyama kutoka Singida Black Stars.

Chanzo hicho kilisema Ibenge alitaka awaone wachezaji wote katika kambi iliyopigwa Arusha, ili ajue ambao ataendelea nao kwa msimu ujao na asiowahitaji wapewe mkono wa kwaheri.

“Anaweza akawa mchezaji wa mwisho kusajiliwa endapo hakutatokea changamoto katika maandalizi yanayoendelea, jambo la msingi ni mipango mikubwa iliyonayo Azam kwa msimu ujao, katika Kombe la FA, CAF na Ligi Kuu,” kilisema chanzo hicho.