MABINGWA wa Ligi Kuu ya Zimbabwe, Simba Bhora FC wako kwenye hatua za mwisho za kumalizana na aliyekuwa Kocha wa Mbao FC na Alliance za Mwanza, Godfrey Chapa ili awe kocha msaidizi.
Simba Bhora FC ni wawakilishi wa Zimbabwe kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao baada ya kutwaa ubingwa msimu uliopita ikiwa ni msimu mmoja tu tangu wapande Ligi Kuu nchini humo.
Taarifa ambazo Mwanaspoti limezinasa ni kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Joel Lupaha ndiye anayemtaka Chapa na amependekeza jina lake kwa mabosi wa timu hiyo kutokana na ukaribu walionao baada ya kusoma pamoja kozi ya leseni ya CAF Diploma B jijini Dar es Salaam.
Chapa ambaye kwa sasa anafundisha timu ya BOT Mwanza, amewahi kuwa kocha msaidizi na wa viungo katika timu za Marsh Queens, Catamine, Mbao, Toto Africans, Pamba jiji na Alliance FC.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chapa alikiri kuhitajika na timu hiyo inayojiandaa na hatua ya awali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku ikiwa inaongoza Ligi ya Zimbabwe kkwa alama 47 katika michezo 24.
“Ni kweli tuko kwenye hatua ya mazungumzo hakuna hatua kubwa iliyopigwa mpaka sasa, tunaendelea kusubiria maamuzi ya mwisho ya viongozi wa klabu. Kwa hiyo mambo yakienda vizuri nitawajulisha,” alisema Chapa.
Ikiwa atajiunga na Simba Bhora FC, Chapa atakuwa miongoni mwa wakufunzi wa Tanzania kuanza kazi katika ligi ya Zimbabwe, jambo litakalosaidia kukuza ushawishi wa wakufunzi wetu katika ligi za Afrika Mashariki na Kusini.
Simba Bhora FC ni klabu mpya yenye historia fupi kutoka Shamva, mkoa wa Mashonaland Central, Zimbabwe. Ilianzishwa mwaka 2008 na ilipanda daraja kuingia Zimbabwe Premier Soccer League mwaka 2023. Msimu wa 2024, timu hii iliandika historia kwa kushinda taji lao la kwanza la ligi kuu nchini humo.