Kagera yapata dawa kufufua soka

BAADA ya soka mkoani Kagera kuonekana limetetereka wadau, makocha na Chama cha Soka (KRFA) wamekuja na mwarobaini wa changamoto hiyo wakiwekeza katika soka la vijana.

Kwa sasa mkoa huo hauna timu ya Ligi Kuu baada ya Kagera Sugar  kushuka daraja msimu uliopita, huku ukiwa hauna inayoshiriki First League, Ligi ya Championship na Ligi Kuu ya Wanawake.

Katika kutafuta suluhu ya changamoto hiyo, kituo cha Bukoba Sports Center kwa kushirikiana na Chama cha Soka Wilaya ya Bukoba (Bufa) na kile cha Mkoa wa Kagera (KRFA) waliandaa ligi ya vijana chini ya miaka 17 na 13 iliyoshirikisha timu nane ili kutambua vipaji na kuviendeleza. Ligi hiyo iliyoanza Julai 5 na kuhitimishwa Agosti 8, mwaka huu ilishirikisha timu za Bukoba Sports Center, Tydo Academy, Chinga Chicago Center, Sokoni FC, Great Lake Sports Academy, Young Boys FC, Green Belt FC, na Kagera United. Ambapo, Great Lake iliibuka mabingwa, Bukoba Sports (mshindi wa pili), na Kagera United (mshindi wa tatu).

Mratibu wa mashindano hayo, Vicent Mashauri alisema aliamua kuanzisha mashindano hayo ili kuwasaidia watoto wacheze soka, kutambua vipaji vyao, kuviendeleza, kuwajengea msingi na kuwaunganisha na timu kubwa nchini.

Mashauri ambaye ni mwanzilishi wa Bukoba Sports Center chenye vijana 35 (22 chini ya miaka 177 na 13 chini ya miaka 13), alisema baada ya kumaliza leseni ya Diploma B ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) aliona atumie ujuzi wake kusaidia soka la mkoa wa Kagera.

“Niliangalia fursa ya kuwekeza kwa watoto kwa sababu tuna changamoto ya kutambua vipaji na kuviendeleza. Nimeona nichukue kituo na lengo ni kuzitambua vipaji na kuviendeleza baadaye tuweze kuzipa nafasi ya kuonekana,” alisema Mashauri.

Aliongeza kuwa; “Mwitikio ulikuwa ni mkubwa watu wamefurahi wameona vipaji na tumeona kwakweli tulikuwa tumechelewa sana. Tunatarajia ligi iwe kubwa zaidi na kufikia kila sehemu kwa ukanda huu wa Ziwa.”

Kocha huyo aliwaomba wadau kujitokeze kusaidia vituo ambavyo vinaanzishwa kwani wakiwekeza kuanzia ngazi ya chini itawasaidia makocha kuandaa watoto ambao watakuwa na ushindani na kuleta tija katika taifa.

“Tumekuwa tukilaumu wachezaji wetu wanafika tu ligi kuu lakini haijulikani wamepita wapi, sasa tunaanzisha hivi vituo kwa lengo hilo kwamba wachezaji angalau wawe na wasifu ili watoke huku na msingi mzuri wapate mwendelezo bora wa kisoka tangu wakiwa watoto,” alisema Mashauri.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera (KRFA), Salum Chama aliwapongeza wadau hao kwa kuanzisha wazo la kuibua vipaji katika mkoa huo na kuviendeleza kwani jambo hilo litatengeneza msingi wa soka na kupata wachezaji wazuri.

“Tumeyashuhudia mashindano yalikuwa mazuri na yamepata mwitikio mzuri, huu ni mwanzo tu tunaamini huko mbeleni yatakuwa mwarobaini wa kukwama kwa soka la mkoa wetu, hivyo sisi tutawaunga mkono kwa kuhakikisha wanapata maeneo ya kuchezea,” alisema Chama.