Dar es Salaam. Mtunzi na mwimbaji wa nyimbo za mbalimbali za hamasa za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ikiwemo ya ‘Tundu Lissu wapeleke mchakamchaka’, George Mwingira amefariki dunia baada ya kupata ajali ya gari.
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kusini, Belle Ponera, Mwingira amefariki dunia Jumapili Agosti 10, 2025 maeneo ya Mikumi mkoani Morogoro baada ya basi alilokuwa amepanda kutoka Songea, Mkoa wa Ruvuma kwenda Dar es Salaam kupata ajali.
Nyimbo nyingine ambayo Mwingira, maarufu ‘MC Mwingira’ amewahi kutamba nayo ni pamoja na ‘No reforms no election’ ambayo ndio ilikuwa kibao chake cha mwisho kukitoa kabla ya kufariki dunia.
Kufutia kifo hicho, Chadema kinaendelea kupata pigo kwa wasanii wake kufariki dunia, ambapo kabla ya Mwingira, Fulgence Mapunda ‘Mwanacotide’ alifariki dunia mwaka 2019 aliyewahi kutamba na nyimbo za ‘Chadema People’s Power’ na ‘Polisi msitupige mabomu Chadema’, akafuata Sara Alex aliyetamba na wimbo ‘Mwamba tuvushe’ aliyefariki dunia mwaka 2022.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Agosti 14, 2025, Ponera amesema; ”Mwingira alikuwa anasafiri kwenda Dar es Salaam, kuhudhuria kesi ya Tundu Lissu (mwenyekiti wa Chadema), tulikuwa tuna mawasiliano naye mazuri lakini ghafla yalikata.”
“Baada ya kuona kimya ilibidi tuanze kutafuta taarifa ya nini kimetokea, bahati nzuri tukaambiwa kuna ajali imetokea lakini wahusika walificha kutoa taarifa. Ndio maana utaona kifo kimetokea Jumapili, taarifa zimepatikana leo,” amesema Ponera.
Ponera amesema haikuwa kazi rahisi kujua kilichompata MC Mwingira, lakini baada ya kutuma timu ya watu waliokwenda hadi Mikumi kisha kutembelea hospitali mbalimbali na kubaini rafiki yao amefariki dunia.
“Tunasubiri taratibu za kipolisi ili kuuchukua mwili wa Mwingira utakaosafirishwa kwenda Songea kwa ajili ya mazishi. Nimewasiliana na familia ya Mwingira hatutachelewa kumzika mpendwa wetu,”amesema Ponera.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia amesema kwa sasa chama hicho kipo kwenye majadiliano na familia kwa ajili ya taratibu za kuutoa mwili wa Mwingira katika Hospitali ya Misheni Mikumi kuusafirisha Songea mkoani Ruvuma.
“Tumepata pigo, Mwingira alikuwa msanii mkubwa wa chama na wimbo wake wa mwisho ulikuwa ‘No reforms no election, tutamkumbuka sana,”amesema Rupia.