Hii ndiyo athari kwa wanafunzi wanaotegemea AI bila kusoma vitabu

Unguja. Licha ya baadhi ya wanafunzi kupata daraja la kwanza katika masomo yao, imeelezwa bado wanakabiliwa na changamoto ya uwezo mdogo wa kung’amua mambo kwa kina.

Sababu kuu inayotajwa ni kutojenga tabia ya kujisomea vitabu, na badala yake kutegemea zaidi Akili Unde (AI).

Hayo yamebanishwa leo, Agosti 14, 2025, na Mkurugenzi wa Idara ya Sekondari Zanzibar, Asya Iddi Issa, wakati wa kupokea maktaba ya sekondari ya wasichana Ben Bella, iliyokarabatiwa na Shirika la Read Tanzania kwa kushirikiana na Karimjee Foundation.

Mkurugenzi huyo amesema licha ya ChatGPT kurahisisha upatikanaji wa majibu, mwanafunzi bila kuwa na utamaduni wa kusoma vitabu hawezi kubadilisha na kukuza maarifa yake.

“Wanafunzi hatupendi kusoma, tunataka kutafuta vitu rahisi. Watu wengi wanasikitika kwa wanafunzi wa sasa hivi, wakiulizwa masuala ya kiuelewa, wengine wana daraja la kwanza lakini bado uwezo wa kung’amua mambo unakuwa changamoto, kwa sababu ya kutopenda kusoma zaidi vitabu na kujiongezea maarifa, badala yake wanategemea ChatGPT.

“Hatusomi kwa sababu tumekariri kwa ajili ya kufaulu. Hatusomi kuona vitu vilivyomo kwenye vitabu na kulinganisha na uhalisia wa kwenye jamii. Kwa hiyo, wanafunzi tunapaswa kujisomea vitabu ili kupata maarifa zaidi,” ameshauri.

Amesema ChatGPT inarahisisha kusoma, lakini iwapo wanafunzi wakitegemea jambo hilo linamfanya kuwa na ufinyu wa maarifa iwapo hatatumia akili yake kwa kusoma vitabu.

“Inakusaidia ikiwa nawe una maarifa ya ziada, ukijua unachokitaka na si kwa ajili ya kufaulu mitihani,” amefafanua.

Mkurugenzi wa Shirika la Read Tanzania, Naemy Sillayo, amesema katika mradi huo wametumia Sh27.440   milioni kuweka madirisha mapya, kukarabati paa, kupaka rangi, kununua kompyuta, kutengeneza samani, kukarabati makabati na kununua vitabu vipya 458 vya kiada na ziada.

Amesema wamekuwa na maono ya kuwawezesha vijana wa kike na kiume kuchangia maendeleo kuanzia ngazi ya familia, hivyo watafikia maono hayo kupitia kuchangia uimarishaji wa elimu bora kwa kuweka mazingira bora ya usomaji, vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwa walimu na wanafunzi.

“Mpaka sasa tumekarabati maktaba za shule 177 katika mikoa 22 ya Tanzania Bara, tumefikia wanafunzi zaidi ya milioni 1.861, tumesambaza kompyuta katika shule 17, vitabu zaidi ya milioni 1.645 na kuwezesha mafunzo kwa walimu 1,119,” amesema Sillayo.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Karimjee, Caren Rowland, amesema maktaba hiyo ya kisasa na vifaa vya kutosha ni mfano halisi wa dhamira ya familia ya Karimjee kuleta mabadiliko yenye maana, ikitambua elimu ni njia kuu ya kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii husika.

“Lengo ni kukuza mapenzi ya kusoma, kuongeza kujiamini na kuwapatia wasichana zana wanazohitaji, siyo tu shuleni bali katika maisha ya kawaida,” amesema.

Kwa upande wake, mkuu wa shule hiyo ya sekondari, Zainab Mbwana Mgunda, amesema shule yao imepata maktaba mpya yenye ubora wa hali ya juu.

Ameeleza kuwa awali walikuwa wakipokea vitabu vingi vya ziada, lakini kupitia maktaba hiyo mpya wamepokea zaidi ya vitabu 400, vingi vikiwa ni vya kiada, ambavyo vitawasaidia wanafunzi kujifunza masuala yaliyo ndani ya mitaala ya kitaifa.

“Suala la kusoma halitakuwa na ugumu tena. Tutafanya mkataba mtandao, hatuna tena sababu ya kwenda mbali kusoma,” amesema.

Mwanafunzi Salama Fahda amesema anajivunia upatikanaji wa maktaba ya kisasa katika shule yao, akiamini kuwa uwepo wa rasilimali hiyo utakuwa chachu ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

Shule ya wasichana ya Ben Bella, ambayo ina zaidi ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwake, kwa sasa ina wanafunzi 1,030 na walimu 48.