Burkina Faso, Madagascar zavuka bahari

BAADA ya kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mauritania, kikosi cha Burkina Faso sambamba na Madagascar iliyoitambia Afrika ya Kati kwa mabao 2-0 zinavuka Bahari ya Hindi kwenda Zanzibar kwa ajili ya pambano la kufungia hesabu za Kundi B litakalopigwa kesho kwenye Uwanja wa Amaan.

Kocha Mkuu wa Burkina Faso, Issa Balbone alisema kosa moja limeigharimu timu hiyo mbele ya Mauritania, licha ya kucheza vizuri huku wakiwa pungufu baada ya nahodha Patrick Bihetoue Malo kutolewa kwa kadi nyekundu dakika chache kabla ya mapumziko.

“Tulianza vizuri mchezo kwa kumiliki mpira na kutafuta nafasi ya kupata bao la kuongoza lakini bahati haikuwa upande wetu baada ya kufanya makosa ambayo yaliyotugharimu,” alisema Balbone na kuongeza;

“Kipindi cha kwanza makosa mawili ndiyo yaliyotuangusha, kitendo cha mchezaji kiongozi kuonyeshwa kadi nyekundu na kuipa faida timu pinzani kupata penalti iliyotuumiza.”

Akizungumzia safari ya Zanzibar alisema wameondoka jana mapema ili kuwahi kuwapumzisha wachezaji wao ili wasifanye makosa yaliyofanyika katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Tanzania na walichelewa kuingia Tanzania na kujikuta wanacheza kwa uchovu na kufungwa mabao 2-0.

“Timu itaondoka asubuhi ya kesho (jana), kwani tutacheza mechi Jumamosi  pambano la kujitoa kwelikweli kwa dakika zote 90 ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.”

Hata hivyo, matokeo ya ushindi kwa Burkina Faso mbele ya Madagascar hayawezi kuisaidia kukata tiketi ya robo fainali kuungana na Tanzania, kwani itafikisha pointi sita tu ambazo zimeshapitwa na Mauritania iliyopo nafasi ya pili ikiwa imeshamaliza mechi zake nne na kukusanya pointi saba.

Madagascar iliyoitambia Afrika ya Kati na kuing’oa michuanoni ndio ina nafasi ya kuibana Mauritania kama itashinda mechi hiyo itakayopigwa saa 2:00 usiku kwani itaiwezesha kufikisha pointi saba pia kwa vile kwa sasa ina alama nne, ingawa uwiano wa mabao ya kufunga na kufunga ndiyo utakaoamua nani aende robo. Katika mechi baina ya Mauriania na Madagascar hakukupatikana ushindi kwa vile zilitoshana nguvu kwa kutoka suluhu.