Geita. Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) mkoani Geita, imeanza uchunguzi wa madai ya vitendo vya rushwa vinavyodaiwa kutokea kwenye kura za maoni za Chama cha Mapinduzi (CCM), baada ya baadhi ya wajumbe kupigwa picha mjongeo wakigawana fedha huku wengine wakidaiwa kupewa rushwa ya chakula.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, James Ruge, ametoa kauli hiyo leo Agosti 14, 2025, wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Amesema kuwa uchunguzi unaoendelea hautaathiriwa na taratibu za chama chochote cha siasa, kwani Takukuru inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, uwazi na bila upendeleo wowote.
Ruge amesema Agosti 2, 2025, kupitia mitandao ya kijamii walipokea picha ya video (mjongeo) inayoonyesha wajumbe wanawake wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), kata ya Nyankumbu, jimbo la Geita Mjini, wakigawana fedha baada ya kumalizika kwa kikao cha kuwanadi wagombea wa ubunge.
Amesema pia kuwa tukio jingine liliripotiwa kutokea Agosti 4, 2025, katika Jimbo la Chato Kaskazini, kata ya Bukome, ambapo wajumbe walipatiwa chakula na vinywaji katika siku ya upigaji kura za maoni.
“Kufuatia matukio hayo na mengine yaliyotendekea, ofisi ilianzisha uchunguzi unaokamilishwa kwa kukusanya ushahidi ili kuthibitisha tuhuma za rushwa dhidi yao,” amesema Ruge.
Akizungumza kuhusu utendaji kazi wa Takukuru, Ruge amesema kuwa taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh700 milioni. Fedha hizo ni sehemu ya mikopo iliyotolewa kwa vyama vya ushirika (AMCOS) vinavyohusika na kilimo cha tumbaku.
Ameeleza kuwa mikopo hiyo ilitolewa na taasisi mbili za kifedha kwa vyama vya msingi vya ushirika katika Wilaya ya Mbogwe, ambapo vyama hivyo vilishindwa kurejesha jumla ya Sh930 milioni.
Amesema baada ya Takukuru kufanya uchambuzi wa mfumo wa usimamizi wa mikopo hiyo, walibaini mapungufu mbalimbali yaliyowezesha urejeshaji wa zaidi ya Sh700 milioni.
Aidha, Ruge amesema kuwa Takukuru mkoani Geita inaendelea na ufuatiliaji wa matumizi ya fedha katika utekelezaji wa miradi 20 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh5.8 bilioni, ambapo baadhi ya miradi hiyo imebainika kuwa na changamoto na mapungufu ya kiuendeshaji.
Akizungumzia utekelezaji wa Programu ya “Takukuru Rafiki”, Ruge amesema kuwa kupitia programu hiyo, barabara ya kutoka Kijiji cha Nzera hadi Gona yenye urefu wa kilomita 2.65 imefanyiwa matengenezo na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura), kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu ubovu wa barabara hiyo.
Vilevile, kupitia programu hiyohiyo, wananchi na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwingiro wameondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji, baada ya kuchimbiwa kisima chenye thamani ya Sh24.9 milioni.
Katika hatua nyingine, Ruge amesema kuwa katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2025, ofisi yake ilipokea jumla ya malalamiko 62, ambapo kati ya hayo 33 sawa na asilimia 53 yalihusu makosa ya rushwa.