Dar es Salaam. Mtiania wa urais kupitia ACT Wazalendo, Luhaga Mpina amesema uamuzi wake wa kuchoma nyavu alipokuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ulitokana na matakwa ya sheria na kwamba alizozichoma zote zilistahili kufanywa hivyo.
Kauli hiyo ya Mpina inafafanua mitazamo ya wanasiasa mbalimbali ambao wamekuwa wakidai, hatua yake hiyo alipokuwa waziri ilihusisha uonevu dhidi ya wavuvi.
Mpina ameyasema hayo leo, Alhamisi Agosti 14, 2025 alipozungumza na waandishi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.
Amesema alipoingia katika wizara hiyo mwaka 2017 alikuta uvuvi haramu umekithiri katika maeneo yote na kuhatarisha maisha ya walaji.
Ingawa nchi ilikuwa na eneo kubwa la maji, amesema Tanzania ilianza kutegemea samaki kutoka nje ya nchi, huku viwanda vikifungwa.
“Watu wanaotaka kuzungumza wasipotoshe waseme nilichoma nyavu haramu. Na vipande zaidi ya milioni moja na watuhumiwa zaidi ya 14,000 walikamatwa,” amesema.
Amesema alizichoma nyavu haramu kwa sababu hazikuruhusiwa kutumika kwa shughuli za uvuvi kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi na kanuni zake za mwaka 2009.
“Mtu anapozungumza alichoma nyavu, alichoma nyavu, ameamua kupotosha tu, bali uhalisia nimechoma nyavu haramu,” amesema.
Katika mazingira hayo ya utendaji, amesema alitambua kuwepo kwa baadhi ya wasaidizi wake wazembe walioonea baadhi ya wavuvi, hivyo aliwashughulikia kwa kuwafuta kazi.
“Kwa kutambua hilo, nilimwelekeza mwajiri awe anatembea na barua ya kuwafukuza kazi maofisa wa uvuvi, atakaowakuta wanaonea wavuvi. Niliwataka wawe wanatembea na barua waache nafasi za kuandika jina na tarehe tu,” amesema.

Mgombea wa nafasi ya urais kupitia ACT – Wazalendo,Luhaga Mpina akizungumza katika mkutano wake na wahariri wa vyombo ya habari,jijini Dar es Salaam.Picha na Michael Matemanga
Kutokana na hatua zake hizo, amesema wingi wa samaki uliongezeka kwa asilimia 95.5 na dagaa waliongezeka kwa asilimia 41, ilhali aliingia akikuta samaki wanaostahili kuvuliwa Ziwa Victoria ni asilimia 3.3 pekee.
Mbali na hayo, Mpina amesema amejiunga na ACT Wazalendo baada ya kujiridhisha kuwa, chama hicho kinatoa jukwaa madhubuti la kufanikisha ajenda ya vizazi vijavyo na ukombozi wa Taifa.
“Hata kabla sijajiunga na ACT Wazalendo, watu wanaumiza kichwa wanachambua wanatoa ushauri wa kitaalamu. Ni chama ambacho nimekuwa nikikifuatilia. Nipo kwenye chama makini na jukwaa sahihi la kuwakomboa wananchi,” amesema.
Kwa upande wa mgombea mwenza wa urais wa chama hicho, Fatma Alhabib Fereji amesema anaamini anashirikiana na Mpina ambaye si mgeni wala jina lake sio jipya na sifa zake za kiuongozi hazihitaji maelezo mengi.
Ameeleza ameshuhudia miaka 20 ya dhamira ya kweli ya Mpina katika kuwatetea, kuwasikiliza na kutafuta suluhu ya changamoto wananchi.
“Mpina ni chuma tena chuma kipya kabisa. Chuma kiaichonyauka, wala kupauka katika kupigania haki na ubadhilifu wa mali za umma,” amesema.

Ameeleza yaliyomkuta Mpina si ajali ya kisiasa bali mapenzi ya Mwenyezi Mungu kumuunganisha na chama hicho cha ACT Wazalendo na hatimaye kuwa mgombea wa urais.
“Maono ya kisiasa ya Mpina yamepata jukwaa sahihi kwani ACT Wazalendo ni nyumba ya watu wanaodai haki. Mpina ni kiongozi imara kwenye kulinda maslahi ya watu,” amesema.