Morogoro. Wilaya ya Kilosa mkoani hapa ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na uharibifu wa misitu unaochochewa na biashara ya kuni na mkaa.
Nishati hiyo inayotumika kwa wingi katika kupikia, husafirishwa kutoka Kilosa kwenda kuuzwa katika miji na majiji mbalimbali nchini.
Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, akizungumzia mikakati iliyowekwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, amesema mkakati wa kwanza ni kuhakikisha misitu ya vijiji vinalindwa.
Amesema mkakati mwingine ni kutafuta wadau watakaotoa elimu ya madhara ya nishati chafu, sambamba na kusambaza teknolojia za kisasa za kupikia zitakazopunguza matumizi ya kuni na mkaa.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa jamii inapaswa kuondokana na mazoea ya kutumia kuni na mkaa na kuhamia kwenye nishati safi, rafiki kwa mazingira na salama kiafya.
“Hivi karibuni Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) walikuja hapa Kilosa na kuleta majiko banifu yanayotumia mkaa kidogo. Yaliuzwa kwa bei ambayo wananchi wanaweza kumudu na kwa kweli wengi waliyachangamkia,” amesema Shaka.
Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka Rea, Advera Mwijage amesema kuna mradi wa usambazaji wa majiko banifu ulioanza Kilosa na baadaye utasambaa nchi nzima.
“Mradi huu unatekelezwa kwenye vijiji na miji. Lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anatumia nishati safi na salama kwa afya na mazingira,” amesema Mwijage.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa Serikali imelipia asilimia 80 ya gharama za jiko, mwananchi hulipa Sh14,700 badala ya Sh73,500.
Pia, kupitia mpango wa kusambaza majiko ya gesi na nishati safi kwenye taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100, Rea imefikisha majiko ya gesi kwenye magereza yote nchini na yameachana na kuni na mkaa.
Fatuma Ally, mama lishe na mkazi wa Mtaa wa Behewa amesema alihamasika kununua jiko banifu baada ya kuliona na kulijaribu kwa ndugu yake.
“Linaokoa mkaa. Kiasi kinachotumika kuiva chakula ni kidogo mno, ukilinganisha na majiko tuliyoyazoea,” amesema Fatuma.
Pia, amefurahia bei nafuu ya Sh14,700 na mfumo wa mauzo unaotumia Kitambulisho cha Taifa (Nida), unaozuia mtu kununua majiko mengi na kuuza kwa bei ya juu.
Fatuma amesema awali alitumia zaidi ya Sh100,000 kwa mkaa kila mwezi, lakini sasa anatarajia gharama kupungua kwa kuwa anatumia gesi na jiko banifu.
Amesema kabla ya kutumia gesi, alikuwa anatumia gunia mbili za mkaa kwa mwezi, lakini sasa matumizi yameshuka hadi Sh50,000.
Amesema baada ya kununua jiko hilo anatarajia kupunguza zaidi gharama.
Fatuma amesema kitu kingine alichopenda ni namna jiko hilo lilivyokuwa imara na namna Serikali inavyouza majiko hayo kwa wananchi kwa kuzingatia utaratibu wa kitambulisho cha Nida kwa kuwa, inasaidia kudhibiti mtu kununua jiko zaidi ya moja kisha kuuza kwa bei ya juu.
Mbali na mikakati hiyo, Wilaya ya Kilosa itanufaika na mradi wa pamoja wa National Carbon Monitoring Centre (NCMC) unaolenga kupunguza uharibifu wa misitu kwa kutoa nishati mbadala kwa shule na jamii.
NCMC kwa kushirikiana na World Food Programme (WFP), imesaini makubaliano ya kutumia umeme kupikia katika shule 50 za msingi na sekondari.
Mtendaji Mkuu wa NCMC, Profesa Eliakim Zahabu, amesema mradi huo unatekelezwa Kigoma, Tabora, Dodoma na Dar es Salaam na baadaye katika wilaya za mkoa wa Morogoro.
“Mradi huu utapunguza matumizi ya kuni na mkaa yanayochochea ukataji wa miti kwa ajili ya chakula cha wanafunzi,” amesema Zahabu.
Mkurugenzi Mkazi wa WFP, Ronald Tran Ba Huy amesema takribani hekta 500,000 za misitu hupotea kila mwaka nchini kutokana na matumizi ya kuni na mkaa.