PURA, MCL kushirikiana utoaji wa elimu ya mafuta, gesi asilia

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na Kampuni ya Mwananchi Commumications Ltd (MCL) zimekutana kujadili ushirikiano katika utoaji wa elimu kwa umma kuhusu masuala ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia Tanzania.

PURA na MCL zimekutana leo Alhamisi Agosti 14, 2025 jijini Dar es Salaam katika kikao kilichohudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni na Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Rosalynn Mndolwa-Mworia.

Akizungunza wakati wa kikao, Mhandisi Sangweni amesema mashirikiano baina ya PURA na MCL ni muhimu na yatasaidia kuongeza uelewa kwa wananchi na wadau mbalimbali kuhusu historia ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini, hali ya uzalishaji wa gesi asilia, miradi inayotekelezwa, fursa zilizopo na mipango ya uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi nchini.

“PURA imekuwa ikitumia vyombo mbalimbali vya habari katika kutoka elimu ya mafuta na gesi asilia kwa umma. Hata hivyo, kuwa na ushirikiano mahususi na Mwananchi Communications kutaongeza tija katika kuwafikia wadau,” amesema Mhandisi Sangweni.

Amesema PURA na MCL zitashirikiana pia katika utoaji wa elimu ya nishati safi na nafasi ya PURA katika kufanikisha ajenda ya Taifa ya kuhamia matumizi ya nishati safi.

Kwa upande wake, Rosalynn amesema mashirikiano ya PURA na MCL yataleta mageuzi katika uhabarishaji wa masuala ya mafuta na gesi asilia hususan suala zima la mchango wa sekta ya gesi asilia na nafasi ya PURA katika kufanikisha lengo la Serikali la kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Rosalynn amesema MCL imeendelea kutoa elimu ya nishati safi ya kupikia kupitia habari, makala maalumu na majukwaa mbalimbali kama vile makongamano.

Kwa upande wa makongano, Rosalynn amesema kongamano la nishati safi ya kupikia linaroratibiwa na MCL. Kongamano hilo litafanyika Septemba 2025 na kuleta pamoja wadau zaidi ya 200 kutoka sekta ya umma na binafsi.