Dodoma. Baadhi ya majina ya wanachama 24 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliochukua fomu kuwania uteuzi wa kugombea ubunge wa Jimbo la Kongwa kufuatia kifo cha aliyekuwa hayati Job Ndugai, yameanza kufahamika, likiwamo la Rais wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said.
Fomu za kuomba kugombea ubunge zilichukuliwa na kurudishwa juzi baada ya CCM kutangaza mchakato huo kufanyika kwa siku moja.
Hersi ni miongoni mwa majina manne mapya yaliyoingia katika orodha ya watiania hao 24, ambao wamejitokeza kuomba ridhaa ya CCM kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025.
Awali, Hersi alikuwa miongoni mwa wagombea waliochukua fomu kuwania kuteuliwa kugombea ubunge wa Jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam, akiwa pamoja na watiania wengine 40.
Kati ya hao waliorejesha fomu walikuwa 39 na mchujo wa vikao vya CCM ulirudisha majina sita kwa wajumbe wa jimbo kupiga kura za maoni huku jina la Injinia Hersi likiwa limechujwa na vikao vya juu vya CCM.
Mbali na Hersi, wengine waliothibitisha kuchukua fomu kwa mara ya pili ni Deus Seif, ambaye katika mchujo wa awali wa Jimbo la Kongwa, alishika nafasi ya tatu kwa kura, nyuma ya aliyekuwa mbunge, Ndugai, aliyekuwa akiongoza kwa kura nyingi.
“Ni kweli nimechukua fomu baada ya kutangazwa na chama chetu, hata hivyo siwezi kufanya chochote wala kusema neno lolote hadi tutakapopata maelekezo ya chama,” amesema Seif.
Mtiania mwingine ni Elias Mdao ambaye katika matokeo ya awali alikuwa nafasi ya sita kati ya 10 waliokuwa wameingia kwenye kura za maoni.
Katibu wa CCM Wilaya ya Kongwa, Joyce Mkaugala alipoulizwa majina ya waliochukua fomu alitaja jina moja la Hersi huku akiahidi kutaja mengine baadaye atakapomaliza kikao.
Amesema mchakato wa vikao bado unaendelea, lakini kila hatua itafanyika kwa haki kwa mujibu wa kanuni za chama.
“Ni watu 24 kama mlivyosikia, Injinia Hersi Said kweli ni miongozi mwa watiania waliojitokeza kuomba uwakilishi wa jimbo hili,” amesema Mkaugala.
Alipoulizwa kuhusu hatua gani zinafuata baada ya hapo, Mkaugala amewataka waandishi wa habari kusubiri taratibu za chama watajulishwa hatua itakayofuata.
Hersi anaungana na wagombea wengine kuomba nafasi kwa mara ya pili katika uchaguzi huu tofauti ikiwa ni yeye awamu ya kwanza aliomba Jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam ambako jina lake halikurudishwa na vikao vya uteuzi sasa anawania Kongwa mkoani Dodoma.
Mmoja wa wagombea Paschal Mahinyila amedai kukiukwa kwa utaratibu na baadhi ya watiania ambao wamejaziwa fomu za kuomba kuteuliwa kugombea.
Mahinyila amedai kwa ushahidi walionao fomu za mmoja wa watiania zilijazwa na mtu mwingine anayetajwa kuwa mjomba wake (jina limetajwa).
“Taarifa tumezitoa kwa wakubwa huko juu, haiwezekani mtu anamtuma ndugu kumchukulia fomu halafu inakuwaje mtu unakwenda kufoji saini, hilo ni kosa,” amedai Mahinyila.
Machakato kabla ya kifo cha Ndugai
Kwa mujibu wa taarifa, idadi kubwa ya majina yaliyochomoza ni kundi la wanachama waliogombea na Ndugai ambao majina yao yalipenya kwenye mchujo na wale ambao hawakupita kwenda kwa wapigakura nao wamo.
Waliopitishwa mchujo wa awali na kura zao katika mabano ni Ndugai (marehemu) aliongoza kwa kura 5,692, Isaya Mngurumi (2,602), Deus Seif (1,260), Dk Samora Mshang’a (544), Dk Simon Ngatunga (517), Elias Mdao (435), Philip Chiwanga (558), Paschal Mahinyila (331), Balozi Emmanuel Mbennah (232) na Ngaya Mazanda (195).
Kurudiwa kwa mchakato huo wa kura za maoni umetokana na kifo cha Ndugai kilichotokea Agosti 6, 2025, siku mbili baada ya kufanyika kwa kura za maoni, na alizikwa Agosti 10, 2025, kijijini kwao wilayani Kongwa.
Kufuatia msiba huo, CCM ilitangaza kuanzisha upya mchakato wa kumpata mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika Jimbo la Kongwa.
Agosti 12, 2025 Katibu wa CCM Wilaya ya Kongwa, Joyce Mkaugala alikaririwa akisema waliojitokeza kuchukua fomu hadi majira ya mchana walikuwa 24.
Mkaugala pia amesema taratibu za chama zitafuatwa kwa wagombea hao ikiwamo kulipia Sh500,000 kwa kila fomu kama ilivyokuwa awali na kuwa kura za maoni zitapigwa siku ya Jumapili ya Agost 17, 2025.