Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Arusha imetoa semina kwa wadau wa kodi juu ya unafuu wa ushuru wa forodha kwenye malighafi zinazoagizwa nje ya nchi, nafuu inayolenga kuviwezesha viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa kwa gharama nafuu na kushindana bei na zinazotoka nje ya nchi.
Semina hiyo imefanyika leo Alhamisi Agosti 14, 2025, ikihusisha wadau mbalimbali wa kodi ambao wamepewa elimu juu ya unafuu wa ushuru wa forodha.
Akizungumzia nafuu hiyo, Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha, Deogratius Shuma amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha bei za bidhaa za ndani zinakuwa shindani sokoni, ikiimarisha uzalishaji wa ndani na kupunguza uagizaji wa bidhaa nje wakati zinaweza kuzalishwa nchini.

“Tunapotoa unafuu wa forodha kwa malighafi, tunahamasisha uzalishaji zaidi nchini. Matokeo yake, uagizaji wa bidhaa kutoka nje unapungua, kwa kufanya hivi hata matumizi ya fedha za kigeni yanapungua na ajira zinaongezeka,” amesema Awadhi.
Amesema Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inatoa fursa ya misamaha kwa wazalishaji ili kuongeza tija ya uzalishaji na kupunguza gharama.
“Unafuu huu utasaidia bidhaa za ndani kuuzwa kwa bei nafuu zaidi,” amesema.
Akizungumzia hilo, Emily Wilson ambaye ni Mkurugenzi wa fedha wa Cool Package Limited, amesema mabadiliko yaliyofanywa na Sheria ya Fedha ya mwaka 2025 yamegusa taratibu mbalimbali za forodha hususan namna mizigo inavyoingia na kutoka nchini.
“Kupitia semina zetu, tunawapa maofisa na mawakala wa forodha uelewa wa mabadiliko haya na malengo ya Serikali kwa mwaka wa fedha husika. Lengo ni kuhakikisha wote tunakuwa na uelewa wa pamoja na kushirikiana katika ukusanyaji wa mapato,” amesema.

Naye Ofisa Forodha Mkuu wa TRA, Allan Maduhu amesema mafunzo yanayotolewa ni kuwafundisha wazalishaji namna ya kujaza taarifa (return) kila robo mwaka, zikionyesha jinsi walivyotumia malighafi walizonufaika nazo kupitia msamaha wa forodha.
“Serikali inataka kuhakikisha kuwa msamaha huu una manufaa na kuepusha matumizi mabaya,” amesema.