Waliombea eneo kulikotokea ajali iliyoua watu 42 Same

Same. Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini wamekutana katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro na kufanya ibada maalumu katika eneo la Sabasaba, ambako kulitokea ajali mbaya ya barabarani iliyogharimu maisha ya watu 42, Juni 28, 2025.

Katika ibada hiyo, viongozi hao wameiomba Serikali kuweka mnara wa kumbukumbu wenye majina ya wote waliopoteza maisha katika ajali hiyo, wakisema hatua hiyo itasaidia kuhifadhi historia ya tukio hilo na kutoa nafasi kwa familia, jamaa na jamii kwa ujumla kutafakari na kuomboleza kwa heshima.

Wamesema mnara huo utakuwa sehemu ya kumbukumbu ya kudumu, mahali pa sala na tafakari kwa wote walioguswa na tukio hilo.

Ajali hiyo ilitokea baada ya basi la kampuni ya Chanel One lililokuwa likitoka  Moshi kwenda Tanga kugongana uso kwa uso na basi dogo aina ya Coaster lililokuwa likielekea Moshi kutoka Same.

Magari yote yalilipuka moto baada ya ajali, huku abiria wakiwa ndani.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, watu 42 walipoteza maisha, ambapo 31 kati yao walikuwa kwenye basi dogo aina ya Coaster wakielekea kwenye harusi mjini Moshi, huku wengine 11 wakiwa ni abiria wa basi la Chanel One.

Akizungumza baada ya ibada hiyo maalumu ya maombi, Kaimu Sheikh wa Wilaya ya Same, Abbas Hassan amesema kuwa viongozi wa dini wataendelea kufanya maombi katika eneo hilo la ajali pamoja na maeneo mengine ndani ya Wilaya ya Same, ambayo kwa kipindi cha hivi karibuni yamekuwa yakikumbwa na matukio ya ajali za barabarani.

“Viongozi wa dini, tumejizatiti kuendelea na ibada na sala maalumu kwa ajili ya kuombea waliopoteza maisha, kuifariji jamii, na kuiombea wilaya yetu dhidi ya majanga kama haya.

“Tumemuomba mkuu wa wilaya  suala hili la maombi liwe ni endelevu kwa wilaya yetu, lakini kingine ikiwezekana hili eneo lijengwe mnara wa kumbukumbu ya wenzetu wote waliopoteza maisha kwa ajali  iliyoua watu 42,” amesema Sheikh Abbas.

Amesema katika maisha ya hapa duniani anayetuongoza ni Mwenyezi Mungu pekee, hivyo anajua kila mwanadamu ataondoka hapa duniani kwa namna gani.

Kwa upande wake, Mchungaji Amani Mndeme wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), amesema viongozi wa dini wataendelea kufanya maombi ya mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kutokana na wingi wa matukio ya ajali yaliyokuwa yakiripotiwa.

“Tupo mahali hapa ambapo palitokea ajali mbaya sana  ya kihistoria, kwa kuwa ilipoteza maisha ya watu wengi kwa wakati mmoja. Leo tumekusanyika hapa kufanya maombi maalumu. Familia nyingi zimepoteza wapendwa wao; wengine wamebaki yatima, wajane, au wagane. Tuko hapa kuwaombea waliobaki, ili Mungu afungue milango ya faraja na tumaini kwao,” amesema Mchungaji Mndeme.

Ameongeza kuwa viongozi wa dini wanapendekeza eneo hilo liwe na mnara wa kumbukumbu wa kudumu wenye majina ya marehemu, ili isiwe tukio lililosahaulika.

“Hili jambo lisimalizike leo tu. Tumependekeza kuwepo kwa mnara wenye taarifa za waliopoteza maisha hapa, kwa sababu shetani hafanyi kazi katika mahali pamoja tu; ana mawakala kila sehemu. Hivyo, mahali kama hapa panahitaji kuwekwa wakfu na kutunzwa kwa maombi ya mara kwa mara,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa dini mbalimbali Wilaya ya Same, Elizabeth Mchani ameeleza kuwa ajali zimekuwa ni jambo la kawaida wilayani humo, hali inayohitaji hatua za kiroho na kijamii.

“Kila baada ya mwezi au miezi michache, wilaya yetu inashuhudia ajali. Mwaka huu pekee tumeshuhudia majanga mengi, lakini hii ya moto ilikuwa ya kipekee na ya uchungu sana. Tulipoona hili limetokea, hatukutaka kukaa kimya; tuliona ni vyema tukusanyike pamoja, tumuombe Mungu aturehemu, atukumbuke, na atakase wilaya yetu,” amesema Mchani.