ZAMBIA imekuwa timu ya tatu kuaga michuano ya CHAN 2024 baada ya jioni kupoteza mechi ya tatu ya Kundi A kwa kufungwa mabao 3-1 na Morocco.
Ushindi huo wa Morocco umepatikana jijini Nairobi na kuifanya ifikishe pointi sita, huku Zambia ikiwa haina pointi yoyote.
Zambia imezifuata Nigeria na Afrika ya Kati zilizoaga michuano kutoka Kundi na B na D, kwani imesalia mkiani ikiwa na mechi moja ambayo hata ikishinda haiwezi kuwasaidia.
Morocco ilipata bao la kuongoza dakika ya 45 limefungwa na Mohamed Hrimat akipokea pasi ya mwisho ya Youssef Mehri, bao la pili imefunga dakika ya 67 na Oussama Lamlioui akimalizia kwa kichwa pasi ya Mehri na bao la tatu limefungwa Sabir Bougrine dakika 90+5.
Bao la kufutia machozi la Zambia limefungwa dakika ya 70 na Andrew Phiri, huku bao lao jingine lilikataliwa kutokana na aliyefunga alionekana kafanya makosa kabla ya mpira kutinga nyavuni.
Licha ya Morocco kuonekana kuishambulia zaidi Zambia kwa muda wote, lakini ukuta wa timu hiyo haukuwa imara, japo Zambia ilishindwa kutumia udhaifu huo.
Morocco imefikisha pointi 6, imeshinda mechi mbili dhidi ya Angola mabao 2-0, Zambia bao 1-0 imefungwa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wa michuano hiyo Kenya.
Kwa upande wa Zambia imefungwa mabao 2-0 dhidi ya DR Congo, imefungwa mabao 2-1 dhidi ya Angola na imefungwa mabao 3-1 Morocco.
Usiku huu kuna mechi nyingine ya kundi hilo wakati Angola itaumana na majirani zao wa DR Congo.