KLABU ya Yanga itaanza mbio za kufukuzia ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwezi ujao kwa kupangwa kuumana na Wiliete Benguela ya Angola inayotumikiwa na nyota wa zamani wa mabingwa hao wa Tanzania Skudu Makudubela.
Katika kuhakikisha kila kitu kinakaa sawa na kuvaana na kina Skudu, mabosi wa klabu hiyo chini ya kocha Romain Folz imepanga kutesti mitambo mapema ili kuona kama ipo tayari kwa vita ya mechi za kimataifa kabla ya kuifuata Benguela kwao.
Sasa unaambiwa, nyota wapya wa timu hiyo waliosajiliwa na kutambulishwa hitua katika dirisha la usajili litakalofungwa mwezi ujao, Celestin Ecua, Lassane Kouma, Andy Boyeli, Mohamed Doumbia na wengine wanatarajiwa kutesti mitambo kwa anga za kimataifa wakati timu hiyo itakapoikabili Rayon Sports ya Rwanda.
Mastaa hao wapya na wale waliokuwapo msimu uliopita wapo jijini Kigali, Rwanda kukabiliana na wenyeji wao katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayopigwa kwenye Uwanja wa Amahoro, huku kocha wa timu hiyo akitaka kuutumia kusoma namna atakavyotupa karata katika michuano ya CAF.
Yanga imepangwa kuvaana na Wiliete Banguela ya Angola katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazoanza siku chache baada ya Ligi Kuu Bara kuzinduliwa mwezi ujao.
Mashabiki wa mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania leo Ijumaa, wanatarajiwa kushuhudia sura mpya ndani ya kikosi hicho wakiliamsha katika tamasha maalumu ya Rayon.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa mashabiki wa Wananchi kuwaona nyota wapya waliowasajiliwa kwa msimu ujao, akiwemo kiungo mkabaji kutoka Guinea anayetajwa kurithi mikoba ya Khalid Aucho, Balla Moussa Conte, viungo washambuliaji, Lassine Kouma na Mohamed Doumbia na washambuliaji wa kati Andy Boyeli na Celestin Ecua.
Yanga iliyoanza maandalizi ya msimu wa mashindano jijini Dar es Salaam na kucheza mechi moja ya ndani iliyoshinda 4-0 dhidi ya kikosi cha vijana cha timu hiyo, baada ya mechi hiyo itaanza safari ya kwenda jijini Alexandria, Misri kumalizia kambi kabla ya kurejea nchini kuanza msimu mpya.
Katika wiki mbili za maandalizi, Conte, Kouma na Doumbia wameonyesha viwango vinavyotoa matumaini miongoni mwa mashabiki, hasa kwa kuzingatia msimu mpya unatarajiwa kuwa na changamoto za aina yake kwa kocha mpya Romain Folz ambaye kibarua chake ni kutetea mataji ya ndani na kufikisha timu hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mbali na mastaa hao, watakaovaa jezi za njano na kijani kwa mara ya kwanza ni pamoja na Offen Chikola kutoka Tabora United, Abdulnassir Mohammed ‘Casemiro’ kutoka Mlandege na kiraka Abubakar Nizar ‘Ninju’ kutoka JKU wote wa Zanzibar.
Aidha Edmund John aliyejiunga kutoka Singida BS naye anatarajiwa kutambulishwa rasmi leo.
Folz, akizungumza kabla ya mechi, alisema anaona mchezo huu kama kipimo cha kiwango cha wachezaji wake na nafasi nzuri ya kuwapa burudani mashabiki wa timu hiyo.
“Nafurahishwa na juhudi za wachezaji wangu. Nimekuwa nikijaribu mchanganyiko tofauti kwenye safu ya ushambuliaji ili tupate mbinu nyingi za kufunga. Huu ni mchezo wa ushindani, na naamini tutapata nafasi ya kuona mwelekeo wa timu yetu,” alisema Folz.
Kocha huyo pia alisisitiza umuhimu wa kuwapa mashabiki burudani na matumaini mapema kabla ya msimu kuanza.
“Mashabiki ni moyo wa klabu. Tunataka kuwapa furaha si tu kesho (leo) dhidi ya Rayon Sports, bali msimu mzima. Tutaweka nguvu zote kuhakikisha matokeo mazuri yanapatikana,” aliongeza.
Mechi ya leo pia itakuwa fursa kwa Folz kutathmini utimamu wa wachezaji wake kimwili na kimbinu baada ya wiki mbili za mazoezi.
“Ni mechi muhimu ya maandalizi. Wachezaji wote watapata nafasi ya kucheza,” alisema kocha huyo mwenye uraia wa Ufaransa.
Kwa mashabiki wa Yanga, jicho litakuwa si tu kwa matokeo, bali pia jinsi nyota wapya watakavyoshirikiana na wakongwe wa kikosi katika kuwasha moto wa ushindi kuelekea msimu wa 2025/26.
Katika mechi ya leo, Yanga itakosa huduma ya baadhi ya wachezaji wapya, akiwemo Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Mudathir Yahya na Shekhan Ibrahim waliopo timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayoshiriki michuano ya CHAN 2024.