Morocco aita mashabiki Kwa Mkapa

KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amewaita mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Mkapa, kesho Jumamosi wakati timu hiyo itakapokuwa inamalizia mechi za Kundi B dhidi ya Afrika ya Kati, huku akiahidi kuwapa raha kama alivyofanya.

Stars inakamilisha ratiba kwa kuvaana na vibonde hao wa kundi hilo, kwani imeshafuzu robo fainali mapema kwa kukusanya pointi tisa kupitia mechi tatu ilizocheza, huku wapinzani wao wakiwa wameshaanga mapema kwa kupoteza michezo mitatu iliyocheza hadi sasa.

Kufuzu kwa Stars kwenda robo fainali na kushinda mechi tatu mfululizo ni mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo kwenye michuano ya CAF tangu ilipoanza kushiriki michuano ya CAF na hata hivyo, Morocco amewahakikishia mashabiki kazi haijamalizika.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Morocco alisema licha ya mitazamo ya watu wao wanaamini kundi walilopo ni jepesi na wamekutana na timu laini, lakini ukweli ni Stars imekuwa bora kutokana na timu kufuata maelekezo na timu zote za kundi hilo hazikuwa nyepesi hata kidogo.

“Rekodi tuliyoiandika hatutaki kuitia doa Jumamosi (kesho) tunataka ushindi dhidi ya Afrika ya Kati ili tuendelee kuongoza kundi kama ambavyo tumejipangia tangu mwanzo wa mashindano,” alisema nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kutamba na Coastal Union.

“Mwanzo mzuri katika mechi tatu tulizocheza hadi sasa nafikiri ni kujitoa kwa wachezaji na kufuata maelekezo wanayopewa tuna kila sababu ya kuweka jitihada zetu kuhakikisha tunashinda mchezo ujao,” alifafanua Morocco.

Kocha huyo alisema wanastahili kupata matokeo mazuri, sio tu kwa kumbeza mpinzani wanayetarajia kukutana nao, lakini ni kutokana na aina ya kikosi walichonacho ambacho kina malengo ya kuiwakilisha bendera ya nchi kwa ukubwa wa uandaaji wa mashjindano hayo walioupata.

Morocco alisema Afrika ya Kati sio timu mbaya ameifuatilia katika mechi zote walizocheza anaamini watakutana na mechi ngumu kama zilizopita, lakini wamejiandaa na wapo tayari kuipambania nchi na rekodi waliyoitengeneza.