Wacongo, Gambia waipa jeuri Mbeya City

WAKATI Mbeya City ikiingia rasmi kambini leo Ijumaa kwa maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu, uongozi wa timu hiyo umetambia usajili uliofanywa ukieleza matarajio ni kumaliza nafasi saba za juu.

City iliyorejea Ligi Kuu baada ya kukosekana kwa misimu miwili, imefunga kikosi kwa wachezaji 27 wakiwamo wa kimataifa, Kelvin Kingu na Jeremiah Nkoromon (DR Congo) na Famara Kamala kutoka Gambia.

Wengine waliotua kikosini humo ni; Habibu Kyombo, Yahya Mbegu, Ibrahim Ame, Omary Chibada, Beno Kakolanya, Hamad Majimengi huku ikiwa katika hatua za mwisho kumshusha Valentino Mashaka kutoka Simba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Ally Nnunduma alisema usajili huo na wengine ambao hawajatambulishwa ni sehemu ya uwekezaji mkubwa kwa ajili ya timu hiyo.

“Tayari usajili tumefunga, kikosi cha nyota 27 wakiwamo wapya 15 na waliopanda na timu 12 wameanza kambi na tutajificha huko Mwakaleli kuanzia Ijumaa (leo), chini ya Kocha Mkuu, Malale Hamsini,” alisema Nnunduma na kuongeza;

“Kuhusu suala la bajeti tumejipanga kwakuwa hatutarajii kukwama popote, tunao uwezo wa kulipa mishahara tena kwa wakati, posho na gharama nyingine zote, sisi tunataka tuwadai wachezaji matokeo na sio watudai.”

Kigogo huyo alifichua kabla ya kuanza Ligi Kuu, watakuwa na tukio la Mbeya City Day, Septemba 6 na kabla litatanguliwa na uzinduzi wa jezi, Septamba 1 na watacheza mechi ya kirafiki na moja ya timu kubwa nchini na itatangazwa baada ya kufikia makubaliano.